December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TBS yaombwa kufanya ukaguzi wa nyanya madukani

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira.Online

WAFANYABIASHARA, mafundi umeme na wananchi Mkoa wa Dar es Salaam wameliomba Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kutoa ufafanuzi wa nyaya zinazopaswa kuwepo katika soko ili kuwaondolea mkanganyiko wa matumizi wa nyaya hizo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari, wafanyabiashara na wananchi wamesema kwa namna hali ilivyo sasa ni ngumu kwao kutambua nyaya zipi hususan za uunganishaji wa umeme majumbani zinapaswa kuwepo madukani na nyaya zipi hazitakiwi kuwepo.

Kwa mujibu wa wananchi hao, awali TBS ilitangaza kusitishwa kwa matumizi ya nyaya nyekundu na nyeusi na badala yake, zitumike rangi ya blue, ‘brown’ (ugolo) na kijani kulingana na mahitaji ya soko la kimataifa.

Wamesema kutokana na agizo hilo, baadhi yao waliamua kuachana na matumizi ya nyaya hizo zilizozuiliwa na kununua nyaya zenye rangi iliyopendekezwa, ili kuepuka kuvunja sheria ambayo kimsingi ilitaka agizo hilo kutekelezwa.

Mmoja wa wafanyabiashara hao aliyekuwepo eneo la Karikoo, Juma Hassan amesema cha ajabu licha ya agizo hilo kutolewa na mamlaka hiyo, bado nyaya hizo zenye mchanganyiko wa rangi nyeusi na nyekundu, zimeendelea kuuzwa katika maduka mbalimbali jambo aliloomba lifuatiliwe.

“Hii inatuchanganya sana sisi watumiaji na wafanyabiashara kwa kuwa tunajua kuendelea kutumia nyaya hizo ni sawa na kuvunja utaratibu, tunaomba suala hilo lifuatiliwe ikibidi kufanya ukaguzi katika viwanda vyote vinavyozalisha ili wahusika wabainike,” amesema.

Bila kuvitaja viwanda hivyo, amesema ni wazi kuwa vinakiuka kwa makusudi agizo hilo la TBS, ambayo kimsingi ndiyo chombo cha serikali kilichopewa dhamana ya kusimamia viwango vya bidhaa mbalimbali zinazozalishwa ama kuingizwa nchini.

Hata hivyo amesema, uchunguzi wao wamebaini pia zipo baadhi ya nyaya hizo ambazo zimezuiliwa matumizi huingizwa hapa nchini na moja ya kampuni, hivyo kutaka uchunguzi zaidi kufanyika.

Wamesema kwa sasa nyanya hizo, bado zinaendelea kuuzwa katika baadhi ya maduka hususan yaliyopo Mitaa ya Narung’ombe na Gogo iliyopo eneo la Kariakoo, Dar es Salaam.