November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mbinu shirikishi zinavyosaidia kumaliza migogoro ya ardhi nchini

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

“PAMOJA na Serikali ya Awamu ya Tano kuhamasisha uwezekaji nchini, lakini inawajali wanyonge ili waweze kuishi na kuendesha maisha yao bila bughudha yoyote,’’ hiyo ilikuwa ni kauli ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi wakati wa ziara yake ya alipotembelea mkoani Kilimanjaro.

Ziara hiyo ya siku tatu, siyo tu ilileta neema kwa wananchi katika baadhi ya maeneo kwenye wilaya hizo bali iliondoa chuki na uhasama uliodumu kwa muda mrefu na eneo lingine kwa zaidi ya miaka thelathini baina ya wananchi na wamiliki wakubwa wa mashamba.

Haikuwa kazi rahisi kuondoa chuki kwa baadhi ya maeneo, lakini naweza kusema uzoefu wa waziri mwenye dhamana ya ardhi, William Lukuvi kwa kushughulika na migogoro ya ardhi katika maeneo zaidi ya 120 ndiyo uliochangia kwa kiasi kikubwa kusuluhisha migogoro ya ardhi baina ya wawekezaji au wamiliki mashamba na wananchi wa maeneo husika.

Lukuvi mara nyingi amekuwa mkombozi wa maeneo mengi yenye matatizo ya ardhi nchini kiasi cha kufanya anapoenda katika eneo kwa ajili ya kutatua tatizo wananchi wengi hujitokeza na kuamini kuwa matatizo yao yaliyodumu kwa muda mrefu yataisha kwa haraka baada ya kushindikana kuatatuliwa na viongozi waliopita.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akizungumza na wakazi wa Mabwebande jijini Dar es Salaam waliomfuata kwa ajili ya kutatua migogoro ya ardhi kupitia Program ya Funguka kwa Waziri mwanzoni mwa mwaka jana.

Ni kutokana na hali hiyo, wataalamu wa mipango miji katika kikao chao cha tano cha Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji kilichofanyika jijini Dodoma hivi karibuni walipendekeza Chuo Kikuu cha Ardhi kumtunuku Waziri huyo Shahada ya Uzamivu katika masuala ya ardhi kutokana na ufahamu wake wa masuala ya ardhi pamoja na jitihada zake za kushughulikia migogoro ya ardhi kwa ufanisi.

Ufumbuzi wa migogoro ya ardhi unaofanywa na Lukuvi unajidhihirisha katika maeneo mengi aliyopita ambapo wananchi waliposikia ujio wake walijitokeza kwa matumaini makubwa ya kutatuliwa matatizo yao ya ardhi.

Kikubwa alichokuwa nacho waziri huyo ni kuzieleza pande zinazovutana katika mgogoro ukweli juu ya tatizo husika na usuluhishi wake tofauti na watu wengine wanaopenda kutumia siasa wakati wa kufanya utatuzi wa migogoro mbalimbali, jambo linalofanya wananchi kuelewa ukweli wa tukio na hali ya tatizo na hivyo kuwafanya kuwa wapole wakati wa kushughulikiwa tatizo husika.

Naweza kusema anachofanya Waziri wa Ardhi ni ujasiri wa hali juu ambao siyo tu unapaswa kuungwa mkono, bali kuwa mfano kwa viongozi wengine wanapotaka kushughulika na matatizo ya wananchi, ambao wengi wao wamekuwa wakifanya mambo, aidha kwa kutoelewa ama kusababishwa na kasi ya maendeleo haraka katika maeneo husika huku Serikali ikichelewa kwenda na kasi hiyo.

Hili la wananchi wengi kuwa na imani na Lukuvi limejidhirisha katika Manispaa ya Moshi pale alipokuwa na ratiba ya kukutana nao katika Programu ya Funguka kwa Waziri ambao katika ukumbi wa mkoa wananchi wengi walijitokeza kwa nia ya kutaka kuonana naye jambo linalofanya kujiuliza inakuaje wananchi kuwa na imani na Lukuvi huku kila halmashauri ikiwa na watendaji wa sekta ya ardhi.

Katika ziara yake mkoani Kilimanjaro Waziri wa Ardhi aliwaeleza watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa huo kuwa, haridhishwi kabisa na namna wananchi wanavyosimamisha misafara ya viongozi kwa nia ya kutatuliwa matatizo yao huku watendaji hao wakiendelea kuwepo maofisini bila kushughulika na matatizo ya wananchi.

“Kama watendaji wa Serikali wakiwemo wale wa sekta ya ardhi wangekuwa wanashughulika na matatizo ya wananchi basi tabia ya wananchi kusimamisha msafara ya viongozi kwa ajili ya kushughukiliwa matatizo yao isingekuwepo kabisa,”anasema Lukuvi.

Akiwa katika shamba la Kirari lililopo Kijiji cha Mlongoni ambapo wananchi wanaishi eneo lenye ukubwa wa ekari 347 na Watawa kubakia na ekari 1,063 na Hati ya shamba hilo ikiwa imetolewa kwa mara ya kwanza Oktoba 26, 1950 kwa ajili ya shughuli za ufugaji na kilimo.

Lukuvi alitatua mgogoro wa pande hizo mbili baada ya kukutana na Watawa wa Katoliki na baadaye viongozi wa Kijiji cha Mlongoni baada ya Mahakama ya Rufaa Tanzania kuwapatia ushindi Watawa na hivyo kulazimu wananchi wa kijiji hicho wanaofikia 3,700 kutakiwa kuondoka katika shamba la Kirari.

Lukuvi alienda eneo hilo la Kijiji cha Mlongoni kiichopo Wilaya ya Siha ikiwa ni tofauti kabisa na ratiba ya ziara yake ya kutembelea wilaya za Hai, Moshi na Same katika Mkoa wa Kilimanjaro baada ya kuombwa kufanya hivyo na mkuu wa mkoa huo Anna Mghwira, kufuatia kuwepo hali tete na hofu ya wananchi wa Kijiji cha Mlongoni kuhusiana na hatma yao baada ya uamuzi wa Mahakama.

Katika kikao chake na Watawa wa Katoliki, Lukuvi aliwaeleza kuwa shirika lao ni wamiliki halali wa shamba hilo kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Rufaa na Serikali haiwezi kupingana na maamuzi hayo na kusisitiza anachotaka ni kuangalia namna bora ya kutekeleza hukumu ya Mahakama.

Na kubainisha kuwa, pamoja na ushindi katika kesi hiyo, lakini kulikuwa na haja ya kuangalia namna bora ya utekelezaji wa hukumu hiyo bila kuathiri wananchi wanaoishi eneo hilo ambao baadhi yao wapo kwa muda mrefu huku wengine wakiwa wameuziwa maeneo bila ya kufahamu.

“Ninyi ni wamiliki halali wa eneo hilo kama ilivyoamuliwa na Mahakama ya Rufaa, lakini ili kuweza kufanya kazi kwa amani kwenye eneo hilo ni lazima kutafuta namna bora ya kutekeleza uamuzi wa Mahakama, ni lazima kuwe na win win situation,” anasema Lukuvi.

Ilikuwa vigumu kuwashawishi Watawa kukubaliana na ombi la Lukuvi, lakini baada ya kutumia takriban saa mbili kuwaelewesha namna alivyoweza kushughulika na migogoro ya aina hiyo katika zaidi ya migogoro 120 kwenye maeneo tofauti ya nchi, Watawa walikubali kumuachia kushughulikia utekelezaji bora wa hukumu ya Mahakama.

Uamuzi huo wa Watawa ulimfanya Lukuvi kuenda eneo la tukio na kuzungumzo na wananchi wa kijiji hicho na kuwaeleza hawana haki ya kuwepo eneo hilo na Serikali haiwezi kuingilia uamuzi huo na katika kutekeleza maamuzi ya Mahakama wananchi wanatakiwa kuondoka kwenye shamba hilo ikiwemo kuvunjiwa nyumba zao.

Hata hivyo, Lukuvi aliwaeleza wananchi hao kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali inayowajali wanyonge, hivyo haitakuwa busara kuwaondoa wananchi wanaokadiriwa kufikia 3,700 hasa ikizingatiwa baadhi yao walijenga nyumba kwa kuweka fedha kidogo kidogo.

Katika kutekeleza namna bora ya hukumu ya Mahakama, Lukuvi aliwaeleza wana kijiji kuwa ili suala hilo liishe kwa amani ni vyema wakakubaliana na utaratibu utakaopangwa na Serikali na kubainisha kuwa hatua ya kwanza ni kufanya tathmini katika eneo hilo.

Kwa lengo la kujua idadi halisi ya wakazi pamoja na mali zao ili kuepuka wajanja wachache wanaoweza kujipenyeza kwa nia ya kujinufaisha na kumuagiza Mkuu wa Wilaya ya Siha na timu yake kuanza kazi hiyo mara moja na kusitisha uendelezaji wowote katika eneo hilo hadi hapo utaratibu mzuri utakapofanywa na kufafanua kuwa, uendelezaji wowote utakaofanyika unaweza kuleta athari kwa wana kijiji ambao kwa sasa hawana haki na eneo hilo.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mlongoni, Manase Herman alimshukuru Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa jitihada zake za kutafuta suluhu katika mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka thelathini na kubainisha kuwa, wao kama viongozi wa Kijiji cha Mlongoni wanakubaliana na utaratibu utakaotumiwa na Lukuvi katika kutafuta suluhu ya jambo hilo.

Huku mwananchi mwingine John Ngwandi akitaka Serikali kuangalia namna ya kuwasaidia hasa ikizingatiwa kizazi cha awali kilishatoweka na wengi waliobaki ni wa kuanzia miaka ya sitini.

Aidha, wakati akikutana na wananchi mbalimbali zaidi ya tisini aliokutana nao katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro katika Program ya Funguka kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Mandeleo ya Makazi, William Lukuvi aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi nchini kujisahihisha ili kuepusha mogogoro ya ardhi ambayo imekuwa ikiwaumiza wananchi wengi.

Mbele ya wananchi wengi waliojitokeza kusikilizwa kero zao za ardhi alisema, ni vyema katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano watendaji wa sekta ya ardhi wakaanza kujisahihisha ikiwemo kuweka majalada yote ya ardhi vizuri kabla hajatembelea maeneo yao kinyume chake atawashughulikia wote watakaobainika kukaidi ama kutoweka sawa majalada ya ardhi.

“Mtu yeyote anayetaka kuiangusha Serikali katika masuala ya ardhi tutamuangusha yeye na lazima tutekeleze Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwa vitendo,”alisema Lukuvi.

Akigeukia migogoro ya ardhi, Lukuvi anasema migogoro mingi inayojitokeza sasa ni ile ya miaka ya nyuma ya kuanzia miaka ya themanini na kubainisha kuwa, kupungua kwa migogoro mipya kunatokana na Serikali ya sasa kuweka mazingira mazuri ya kushughulikia masuala ya ardhi.

“Leo watendaji wa sekta ya ardhi wamenyooka na kazi ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuwanyoosha wale wanaoenda kinyume na taratibu na sheria katika kushughulikia masuala ya ardhi,”anasema.

Kuhusu suala la wamiliki wa ardhi kuchukuliwa maeneo yao bila kulipwa fidia, Lukuvi amewahakikishia wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa, Serikali inalipa kipaumbele suala la fidia kwa wale ambao maeneo yao yatachukuliwa na kubainisha kuwa ikitokea mtu hakufidiwa kipindi ambacho eneo lake limechukuliwa, lakini malipo yake yataanza kuhesabiwa pale eneo lilipochukuliwa na kiwango cha fidia kitakuwa kikiongezeka kadiri malipo yake yanavyochelewa.

Wakati wa ziara yake, Lukuvi pia alikumbana na mgogoro mwingine katika mashamba yaliyokuwa ya vyama vya ushirika na kuhodhiwa na baadhi ya watu ambako huko alishangazwa na namna mashamba hayo yalivyomilikiwa na vikundi vya watu wachache huku wakazi halisi wa maeneo hayo, aidha wakitakiwa kuondoka ama kutonufaika na chochote katika mashamba hayo.

Hivi ndivyo Waziri wa Ardhi anavyoweza kukabiliana na migogoro mengi ya ardhi ambayo imekuwa ikileta taharuki kwa wananchi.

Lakini kwa uajasiri wake, taharuki ya walio wengi ilipungua kwa kiasi kikubwa na wananchi kuona kuwa kimbilio ama suluhisho la matatizo yao ya ardhi limebakia kwake, jambo linalompa waziri huyo kazi kubwa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya nchi lengo likiwa kumaliza ama kupunguza kwa kiasi kikubwa migogoro ya ardhi katika awamu hii ya kwanza ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akiwasili eneo la Kijiji cha Mlongoni wilayani Siha mkoani Kilimanjaro alipoenda kushuhudia hali ya mgogoro wa ardhi ilivyokuwa hivi karibuni. (Mpigapicha Wetu).