Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema wizara hiyo inaendelea kukamilisha maandalizi ya kuanza kufundisha somo jipya la historia ya Tanzania kuanzia Julai mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dodoma kufuatia agizo la Rais John Magufuli kutaka somo hilo lifundishwe nchini,Profesa Ndalichako amesema mpaka sasa tayari wizara hiyo imekamilisha kuandaa muhtasari kwa ajili ya somo hilo.
“Baada ya tamko la Rais kuhusiana na somo hilo kufundishwa mashuleni ,tulianza mara moja maandalizi ambapo mpaka sasa tumeshakamilisha zoezi la kuandaa mihtasari kwa ngazi zote.” amesema Profesa Ndalichako na kuongeza kuwa
“Hivi sasa vitabu vinaandaliwa kwa ajili ya kufundishia wanafunzi na tunatarajia hadi kufikia Machi mosi vitabu vyote vitakuwa tayari na kwamba vitabu hivyo vinaandaliwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo wabobevu katika historia ya nchi ya Tanzania ili somo hilo jipya liweze kufundishwa kwa ufasaha mkubwa.”amesema
Profesa Ndalichako amesema,nchi ya Tanzania ina historia kubwa ambayo ikifundishwa kwa vijana nchini itasaidia kuwafanya wawe wazalendo na kulinda rasilimali za Taifa sambamba na kujua namna nchi ilivyopambana katika kujipatia uhuru.
“Somo hilo litafundishwa kwa lugha ya kiswahili kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita ili liweze kueleweka vizuri kwa wanafunzi .
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Leonard Akwilapo amesema kidato cha tatu ,cha nne na kidato cha sita hawatafanyia mtihani mwaka huu isipokuwa wale wa kidato cha kwanza na cha pili ndio watafanyia mtihani somo hilo.
More Stories
Mhandisi Samamba awasisitiza maafisa madini kusimamia usalama wa migoni msimu wa mvua
Wapinzani kutimkia CCM ishara ya ushindi Uchaguzi Serikali za Mitaa
Vikundi Ileje vyakabidhiwa mikopo ya asilimia 10, DC Mgomi avipa somo