November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Zijue sababu na faida za ukaguzi wa magari kufanyika nchini kwetu

Na ReubenKagaruki,TimesMajira,Online, Dar

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limetaja sababu mbalimbali ambazo zimefanya shirika hilo kuamua kuanza kufanya ukaguzi wa magari hapa nchini, badala ya nje kama ilivyokuwa ikifanyika tangu mwaka 2002.

Mikataba ya mawakala waliokuwa wakifanyakazi hiyo ya ukaguzi wa magari nje ya nchi inatarajia kumalizika mwezi ujao.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa TBS, Lazaro Msasalaga, amesema uamuzi huo umetokana na maombi ya wadau mbalimbali waliotaka ukaguzi huo ufanyike nchini badala ya nje.

“Kimsingi wadau wenyewe ndiyo asili ya haya maamuzi, katika mikutano ambayo tumekuwa tikiifanya na Serikali katika ngazi mbalimbali wamekuwa wakisema kwamba wanasumbuka na kuingia gharama kwa ukaguzi kufanyika nje ya nchi, hivyo baada Serikali kusikiliza malalamiko hayo ikasema hatuwezi kujenga uwezo huo ukaguzi ukawa unafanyika nchini?” amesema Msasalaga.

Amesema Serikali haikuamua tu kufanya ukaguzi huo nchini, bali ni baada ya kusikia kilio cha wadau.

Miongoni mwa wadau uliopendekeza utaratibu huo ni pamoja na waagizaji wa magari, wadau wa bandarini kwa maana ya taasisi binafsi kama wakala wa meli, wakala wa forodha, taasisi za Serikali kama TRA, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari na nyingine za udhibiti na wote wanatakiwa wafahamu programu hiyo itafanyika namna gani.

Faida za ukaguzi kufanyika nchini

Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS, Lazaro Msasalaga

Msasalaga amesema zipo faida nyingi za kaguzi hizo kufanyika nchini ambazo ni pamoja na kuhamishia ajira nchini na kuongeza mapato ya Serikali.

Amesema wanaamini kwamba kwa ukaguzi huo kufanyika nchini, bado TBS watafanya vizuri pamoja na kwamba inapoanza programu yoyote haiwezekani kukosekana changamoto.

“Kwa hiyo kwa vyovyote vile kwa kuanza changamoto zinaweza kuwepo, lakini suala la msingi hapa ni namna gani tutaanza na ni kwa jinsi gani changamoto zitakazojitokeza zikatavyopatiwa ufumbuzi ili utaratibu uweze kufanyika kwa ufanisi,” amesema Msasalaga.

Lakini pia anasema hatua hiyo itatusaidia kujengea uwezo wa Watanzania.

“Lakini tumejifunza hata wakati wa Corona kaguzi hizo nje ya nchi zimeathirika, lakini kama wewe ungekuwa tayari una uwezo ndani ya nchi katika hayo mazingira ugeweza kuweka mazingira tofauti ya ukaguzi,” amesema Msasalaga.

  • Siri ya ufanisi

Amesema ili kuwe na ufanisi ni lazima wadau wote wanaohusika na uagizaji na uondoshaji wa magari bandarini pamoja na mifumo ya bandari yenyewe iweze kusaidia kuhakikisha utaratibu huo unafanikiwa.

Amefafanua kwamba wanapoanza kukagua magari hapa nchini, watu wanaweza kujiuliza kama utaratibu huo utakuwa unaingiliana na taratibu za ushushaji magari kwenye meli.

Utaratibu wa ukaguzi

Ukaguzi utakavyokuwa ukifanyika

Msasalaga amesema utaratibu wa ushushaji magari kwenye meli utabaki kama ulivyo, kwani wakianza kuingilia mchakato wa ushushaji magari na kuingiza kwenye ukaguzi kwa vyovyote vile watachelewesha meli kushusha magari na kuondoka, hivyo kwa nchi ni hasara.

Amefafanua kwamba magari yatashushwa kwa utaratibu uliopo kutoka kwenye meli na kwenda kuwekwa eneo la maegesho ambalo limepangwa ndani ya bandari.

“Na pale bandarini kutakuwa na maeneo manne na tutakuwa na eneo moja nje ya bandari,” amesema na kwamba Yadi ya kwanza ndiyo inayochukua magari mengi madogo na ndiyo eneo meli za magari zinashusha.

Amesema hiyo Yadi ikijaa magari madogo uhamishiwa Yadi ya pili ambayo ipo upande zinaposhushia meli za mafuta. “Lakini karibu na hiyo hiyo Yadi, kuna Yadi mbili za kuhifadhi magari makubwa.

Ukiangalia kwa utaratibu namna magari yatakuwa yanashushwa na kuwekwa ndani ya bandari, sisi TBS tutakuwa na seti 12 za vifaa vya ukaguzi wa magari.”

Seti za vifaa vya ukaguzi

Amesema kati ya seti hizo 12 za vifaa vya ukaguzi, nane zitafungwa kwenye Yadi ya magari madogo na Yadi mbili za magari makubwa kila moja itakuwa na seti moja ya vifaa vya ukaguzi.

Amesema seti moja itafungwa kwenye Yadi ya Kitopeni kwa ajili ya magari machache yatakayohamishiwa huko. “Kwa hiyo tumehakikisha kwamba ndani ya bandari maeneo yote ambayo yanaegeshwa magari kutoka nje yatapata huduma ya ukaguzi bila kujali gari ni kubwa au ndogo,” amesema Msasalaga.

Ameongeza kuwa ujumla ya seti za vifaa vya ukaguzi zitakazokuwa bandarini ni 11 na kwamba ya 12 haitafungwa bandarini, kwani wameishapata eneo UDA ambapo magari ambayo yatakaguliwa na kushindwa kukidhi matakwa ya viwango yatakuwa yakikaguliwa baada ya kufanyiwa matengenezo.

Uondoshaji magari

Msasalaga amesema wakati huo huo mawakala watafanya taratibu zao za uondoshaji magari bandarini kama kawaida hadi wapate vibali.

Ukaguzi

“Na hizo gari zitakaguliwa wakati zimeruhusiwa kutoka zikiwa zimemaliza taratibu zote za kiforodha na hapo ndipo zinapita kwenye hivyo vifaa vya ukaguzi,” amesema Msasalaga na kuongeza;

“Kwenye ukaguzi kuna matokeo ya aina mbili, kama litakidhi kiwango au hapana, kwa vyovyote vile magari yote yatatoka bandarini, lakini lile ambalo limekidhi viwango vya ubora lenyewe litaendelea na utaratibu mwingine unaostahili, kwa lile ambalo litakuwa halijakidhi litatoka bandarini kwa masharti kwamba linakwenda kutengenezwa na baada ya hapo lenyewe litapelekwa eneo la UDA kwa ajili ya kukaguliwa ambapo watakuwa wameweka seti moja ya hivyo vifaa vya ukaguzi.”

Alisema gari lolote halitaruhusiwa kuingia kwenye matumizi hadi lipimwe na kupatiwa cheti ya kukidhi matakwa. Alisema kwa sasa wanakamilisha taratibu za uwekaji vifaa ili zoezi liweze kuanza.

Gharama za ukaguzi

Alipoulizwa gharama za ukaguzi, Msasalaga alisema kwa nje ya nchi zilikuwa dola 150 ambapo TBS ilikuwa inapata asilimia 30, hivyo kwa ukaguzi kufanyika nchini gharama zitakuwa dola 140 na zitaongezeka sh. 30,000 gharama za Service Charge.

“Kwa hiyo haitofautiani na bei ambayo ilikuwa ikitoozwa nje,”amesema.

Uwezo wa kukagua magari

Alipoulizwa kuhusu uwezo wa ukaguzi wa magari ilionao TBS, Msasalaga alisema kila seti ya vifaa vya upimaji magari muda wa wastani wa juu kupima gari moja ni dakika 15.

“Kama kwa seti zote 12 maana yake ndani ya robo saa tunakuwa tumekagua magari 12 na saa moja ni magari 48,” amesema. Kwa hesabu hesabu ndani ya saa 24 TBS itakuwa imekagua magari 1,152.

***Uwezo wa kutoa magari

Amesema kwa upande wao uwezo wa kutoa magari kwa wakati upo kwa asilimia kubwa. Alisema changamoto ambayo itabidi waiangalie ni ya mawakala wanaohusika na utoaji magari kwani mara nyingi magari yakishashushwa walio wengi wanataka kuanza kuyatoa mchana ili yasafiri usiku, hayo ni baadhi ya mambo watayaangalia .