November 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DPP awaburuta mahakamani wanaotumikisha walemavu

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira Online, Dar es Salaam

OFISI ya Taifa ya Mashtaka (DPP) imeridhia kufunguliwa kwa mashtaka dhidi ya watuhumiwa 13 wanaodaiwa kusafirisha watu wenye ulemevu kutoka mikoani na kuwapeleka Dar as Salaam kwa ajili ya kazi ya kuombaomba katika maeneo mbalimbali.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kuwashurutisha watu wenye ulemavu kufanya shughuli hiyo kwa lengo la kuwanufaisha kiuchumi baadhi ya wahalifu waliohusika na uhalifu huo.

Taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari jana na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga imeeleza kwamba ushahidi uliokusanywa unaonesha watu hao kuhusika na tuhuma hizo.

DPP Mganga amesema mara baada ya kupitia jalada husika, alibaini kuwa watu hao wenye ulemavu, watoto wadogo na baadhi wakiwa na ulemavu wa akili walikuwa wamehifadhiwa katika nyumba za kulala wageni zilizopo Tandale zilizotambuka kwa majina ya Kolini, Madiba na Mbokumu mali ya Sadikiel Metta.

Amesema kwenye nyumba hizo walikutwa watu wenye ulemavu 23. Kwa mujibu wa taarifa ya DPP kati ya walemavu hao, wanawake walikuwa nane, wanaume tisa na watoto sita na kwamba wote walikuwa wanatumikishwa katika biashara haramu ya kuombaomba mitaani.

“Watuhumiwa waliohusika na uhalifu huu takribani 13 walikuwa wakiwasukuma watu hao wenye ulemavu kwa kutumia baiskeli maalumu kujipatia pesa katika biashara hiyo haramu,” ameeleza DPP kupitia taarifa hiyo.

Amesema nyumba hizo za kulala wageni hazikuwa na miundombinu rafiki kwa ajili ya watu hao wenye ulemavu. Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwa nyumba ya kulala wageni ya Madiba haikuwa na leseni ya kufanya biashara ya kulaza wageni na hivyo kukwepa kodi na tozo mbali mbali za Serikali.

“Wapo watu ambao walikuwa wakiwasafirisha watu wenye ulemavu kutoka mikoa mbalimbali na kuwaleta Dar es Salaam kwa ajili ya shughuli hiyo.

Kama ilivyoelezwa, watu hao walipokelewa na kupewa hifadhi na Metta kwa lengo la kujipatia kipato kutoka kwenye biashara hiyo haramu,” ilieleza taarifa hiyo.

Amesema watuhumiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kujihusisha na uhalifu wa kupangwa kinyume na sheria, usafirishaji haramu wa binadamu kinyume Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu, kushindwa kulipa kodi kinyume na Sheria na Kuisababishia Mamlaka ya Serikali hasara kinyume na Sheria ya Kuzuia Makosa ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa.

Mashtaka mengine ni ya utakasishaji fedha haramu kinyume na Sheria ya Kuzuia Utakasishaji Fedha Haramu.