November 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lule ataka Mbeya City mpya

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KOCHA mkuu wa kikosi cha Mbeya City, Mathias Lule ameweka wazi mpango wake wa kutaka kukisuka upya kikosi chake ili kufanya mambo makubwa katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) na kuweza kujinasua katika hatari ya kushuka daraja.

Kocha huyo ameweka wazi mpango huo mara baada ya mchezo wao wa ugenini dhidi ya Gwambina FC uliochezwa juzi kwenye uwanja wa Gwambina Complex na kuambulia alama moja kufuatia sare ya goli 1-1 ambapo timu hiyo ilipata goli la kwanza dakika ya 33 lililofungwa na Prosper lakini wenyeji walisawazisha dakika ya 90 kupitia kwa Mayungu.

Matokeo hayo yamewafanya timu hiyo kusalia katika nafasi ya 17 kwenye msimamo wa Ligi wakiwa na alama 13 ikiwa ni timu yenye idadi ndogo ya mechi za ushindi kwani hadi sasa wameshinda mechi mbili pekee dhidi ya JKT Tanzania na Kagera Sugar.

Mbali na kushinda mechi mbili, katika msimamo huo Mbeya City wamepata sare saba na kupoteza mechi nane, nne wakipoteza mfululizo mwanzoni mwa msimu huu lakini pia wameruhusu goli 20 na wao kufunga goli sana.

Kocha Lule ameuambia Mtandao huu kuwa, licha ya kuwa ana muda mfupi ndani ya timu hiyo lakini wachezaji wake wameonesha wana kitu kikubwa na ikiwa watafanyia kazi mapungufu aliyoyabaini katika kipindi hiki cha dirisha dogo basi wanauwezo wa kupata matokeo bora zaidi katika mechi zao zijazo za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.

“Kwa kiwango walichokioneha wachezaji na ikiwa tutafanya maboresho ya baadhi ya nafasi basi tutarajie kupata matokeo tofauti hasa ya ushindi katika mechi zetu zijazo za Ligi kwani tutatumia kipindi hiki kufanyia kazi makosa ambayo nimeyaona kwa wachezaji ikiwemo kutumia ipasavyo nafasi za mabao walizozitengeneza,”.

“Nimeona katika mechi zilizopita nyingi tumekuwa tukifungwa lakini pia wachezaji wamekuwa wakipoteza nafasi nyingi hivyo sasa ni wakati wa kufanya kile tunachokiona ni sahihi kwa maendeleo ya timu yetu, ” amesema kocha Lule.