Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ leo watakuwa na kibarua kigumu mbele ya Uganda katika mchezo wa fainali wa michuano ya CECAFA inayofanyika nchini, Rwanda.
Serengeti Boys ilifanikiwa kutinga hatua hiyo na kufuzu kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON U-17) kwa ushindi wa penalti 4-3 dhidi ya Ethiopia baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya goli 1-1 huku Uganda wakiwafunga goli 1-0 timu ya Taifa ya Djibouti.
Katika mchezo huo, timu hiyo imepanga kulipa kisasi baada ya timu ya Taifa ya Uganda chini ya umri wa miaka 20 kuwafunga kaka zao Ngorongoro Heroes goli 4-1 katika mchezo wa Fainali za CECAFA U-20 uliochezwa Desemba 2 kwenye Uwanja wa Black Rhino, Karatu katika mchezo wa kukamilisha ratiba ya michuano hiyo kwani tayari timu hizo mbili zilikuwa zimeshafuzu kuziwakilisha nchi zao katika Fainali za U-20 za Afrika (Afcon U-20) zitakazofanyia nchini Mauritania 2021 .
Akizungumza kuelekea mchezo huo, kocha mkuu wa timu hiyo, Hababuu Omar amesema kuwa, kikosi chao kitaingia katika mchezo huo na morali ya hali ya juu ili kutimiza malengo yao ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Amesema kuwa, tayari wameshafanyia kazi makosa kadhaa waliyowafanya wachezaji wao katika mchezo wao uliopita hasa katika safu ya ulinzi na ya ushambuliaji kwa kusaidiana na msaidizi wake Maalimu Salehe, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Mirambo pamoja na viongozi wengine wa benchi la ufundi.
Kocha huyo amesema kuwa, kinachowapa matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo ambao wanaamini utakuwa mgumu ni madhaifu waliyoyaona kwa wapinzani wao kwani wameshayafanyia kazi na watahakikisha wanayatumia kuwaadhibu.
“Licha ya kutokuwa na muda wa kutosha lakini tumejitahidi kufanyia kazi makosa kadhaa ambayo tuliyaona kwenye mechi yetu iliyopita ili kujiweka sawa na kupata matokeo mazuri hivyo tunaamini licha ya kuwa na mchezo mgumu lakini tutapata ushindi na kutwaa ubingwa wa mashindano haya,” amesema kocha huyo.
Itakumbukwa kuwa, Serengeti Boys ilipata nafasi ya kushiriki kwenye Fainali za AFCON kwa vijana chini ya miaka 17, mwaka 2017 zilipofanyika nchini Gabon pamoja na mwaka jana ambapo mashindano hayo yalifanyika hapa nchini.
More Stories
Watumishi wa Fahari wafanya Bonanza
Rais Samia atia mkono mchezo wa masumbwi Tanzania
Chino bingwa mpya wa IBA Intercontinental Championship