November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mavazi yasiyo na staa tishio ajira wahitimu vyuo vikuu

Na Tiganya Vincent,TimesMajira Online, Tabora

WANAVYUO wametakiwa kuvaa mavazi yenye staha na yanayozingatia maadili ya ili kuwa kioo kizuri kwa jamii inayowazunguka.

Wito huo umetolewa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo kwenye mahafali ya 38 ya Chuo cha Ardhi Tabora baada ya kuwaona baadhi ya wahitimu wa kike wakiwa wamevaa nguo zisizo na staha.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo(katikati) akiiwa na viongozi wengine wakiimba jana wimbo wa taifa wakati wa sherehe za mahafali ya 38 ya Chuo cha Ardhi Tabora .Picha na Vincent Tiganya

Amesema hata katika utumishi wa umma kuna kanuni za mavazi ambazo mtumishi anatakiwa kuzifuata na kwa wanachuo ni vema wakavaa nguo ambazo zina staha kwa kuwa nao ni watumishi watajariwa.

“Mimi kama mzazi niseme tu tuangalie tulivyo walimu wametufundisha tumepata elimu muda tuliokaa tubadilike… ‘the way you dress’ inakuonyesha ulivyo…hata tukisema mtoe majoho sasa hivi ni aibu tupu wengi mtaabika, lazima mbadilike mvae vizuri” amesisitiza.

Amesema baadhi ya wahitimu nguo walizovaa zinaweza kuwasababishia kukosa ajira kwa kuwa ni kielelezo cha walivyo na hata wakipewa kazi jinsi watakavyokuwa.

“Hata hivi sasa tukisema tuwatenge kwa ajili ya usahili wa kutafuta wahitimu wa kuwapa ajira kuna baadhi yenu tutawaachia kwa jinsi walivyoovaa… lazima uangalie ulivyokuja kutoka kwenu ulikuja vipi na leo unaondoka na tabia gani ? …tubalike tunatakiwa kuonekana kwa kumuonekano mzuri” aliongeza.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi. Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo amewataka wahitimu wa astahahada na stashahda watakaopata fursa ya ajira kuwa waadilifu na wazalendo na kuepuka tamaa ya kupata utajiri wa haraka ambao utawasababishia kuishia kifunguni.

“Ule mtazamo wa kusema nataka kutajirika haraka mafaili yapotee utafungukwa…epukeni vitendo vya wizi, dhuluma, ubadhilifu, kuomba na kupokea rushwa …fanyeni kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozi ya taaluma zenu” alisema.

Makondo aliwataka kutumia ujuzi waliupata kwa ajili ya manufaa ya umma huku wakizingatia kuwa ardhi ndiyo jukwa la maendeleo na tegemeo la kila mtanzania.

Wakati huo huo Katibu Mkuu huyo ametoa wito kwa Halmashauri zote nchini kutumia Chuo cha Ardhi Tabora na kile cha Morogoro katika kupanga matumizi bora ya ardhi kwa kupima mashamba na viwanja na kuvimilikisha.

Amesema hatua itasaidia kuondoa migogoro ya kila siku miongoni mwa wananchi na kuwawezesha kuiongezea thamani ardhi yao na kuwa mtaji wa kuwaletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Naye Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora Biseko Musiba alisema kuwa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wataalamu wa sekta ya ardhi hasa katika ngazi ya mafundi sanifu, wameongeza idadi ya wanachuo.

Alisema katika mwaka wa masomo wa 2020/21, Chuo kinaendesha mafunzo kwa wanachuo 1,446 ikiwa ni ongezeko la wanachuo 174 ukilinganisha 1,272 wa mwaka uliopita wa masomo.