November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Profesa Mkumbo: TIC iwe sehemu ya kufikia malengo ya Serikali

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira,Online, Dar

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais (Uwekezaji), Prof. Kitila Mkumbo, amekitaka Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kuwa chachu ya kufikia malengo ya Serikali ya kufikia asilimia 8 ya pato la taifa sambamba na kuzalisha ajira milioni 8 katika kipindi hiki cha awamu ya pili ya uongozi wa Rais Dkt.John Magufuli.

Prof.Mkumbo ametoa agizo hilo katika kikao na Menejimenti na wafanyakazi wa kituo hicho jijini Dar es Salaam hivi karibuni mara baada ya kufanya ziara yake ya kwanza tangu kuteuliwa kushika wadhifa huo.

Amesema TIC ina jukumu kubwa kuhakikisha wanavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza nchini ili kufikia malengo ya Serikali ya kujenga uchumi wa viwanda ifikapo 2025.

“Malengo ya Serikali ni kufikia asilimia 8 ya pato la taifa na kuhakikisha uchumi wetu unazalisha ajira milioni 8, hivyo kila mtumishi ana wajibu wa kutekeleza majukumu yake ili malengo yaweze kutekelezeka na kuifanya nchi yetu kuwa na maendeleo endelevu,” amesema Prof.Mkumbo

Ameeleza kuwa TIC iwe mwezeshaji katika kurahisisha usajili wa miradi mbalimbali ya wawekezaji jambo litakalovutia zaidi wawekezaji kuja Tanzania na kufanya uwekezaji kupitia fursa mbalimbali zilizopo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Nchini(TIC) Dkt.Maduhu Kazi (kushoto) akieleza jambo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais(Uwekezaji) Prof.Kitila Mkumbo(kulia) alipofanya ziara kutembelea kituo hiyo jijini Dar es Salaam hivi karibuni kujionea utendaji kazi wa kituo na kuzungumza na wafanyakazi juu ya kutekeleza wa jibu wa kuhamasisha uwekezaji nchini. Na mpicha pocha wetu.

“Tanzania ipo katika mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji ikiwa ni pamoja utulivu wa kisiasa, maboresho ya sera, sheria na kanuni za uwekezaji pamoja na uhakika wa soko kutokana na nchi kuwa mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini wa Afrika ni sehemu ya vivutio,” amesema Prof.Mkumbo.

Ameongezea kuwa maboresho ya mifumo ya elimu yamepelekea kuwepo kwa wafanyakazi wenye weledi pamoja na gharama za nguvukazi kuwa rafiki ni sehemu ya mazingira wezeshi kwa wawekezaji kuvutiwa kuwekeza, hviyo ni jukumu la TIC katika kujipambanua kwa wawekezaji ndani na nje ya nchi ili waweze kupata taarifa hivi.

Katika hatua nyingine Prof. Mkumbo ameitaka TIC kuimarisha uratibu wa mahusianao na taasisi nyingine za Serikali ili utoaji wa huduma za usajili wa miradi ya wawekezaji ifanyike kwa urahisi pasipo na vikwazo vyovyote hali itakayoiweka Tanzania kwenye nafasi za juu kwenye orodha ya nchi zenye mazingira wezeshi ya uwekezaji duniani.

“Muhimu kwa mamlaka zetu kuwa na utaratibu maalum wa kwenda kufanya ukaguzi kwa wakati mmoja ili kupunguza muda wa kaguzi za mara kwa mara kwa kila taasisi jambo linalokwamisha uzalishaji, hivyo tukiboresha hili tutazidi kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kuchochea uwekezaji,” amesema Prof.Mkumbo

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dkt. Maduhu Kazi alimshukuru Waziri kwa kutembelea ofisi yake na kutoa maagizo mbalimbali hususani suala la kujitangaza ndani na nje ya nchi juu ya kuvutia wawekezaji.

“Tutayafanyia kazi maagizo yote ya Serikali ikiwa ni pamoja na kubadili mtazamo wa watenda kwa wawekezaji jambo litakalo jenga urafiki na urahisi katika kufanikisha usajili wa miradi ya mbalimbali nchini,” amesema Dkt.Kazi

Dkt.Kazi aliongezea kuwa kituo chake kitakuwa kiunganishi kati ya Serikali na wawekezaji ili kuratibu kwa urahisi zoezi la usajali wa miradi ya uwekezaji husasani viwanda ili malengo ya Serikali ya kuzalisha ajira milioni 8 iweze kutimia.