November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkufunzi wa zana za Kilimo kutoka Mamlaka ya Elimu na ufundi stadi VETA,Mhandisi Joseph Kimako akiwasilisha mada ya nyanya katika Mkutano wa Wahandisi mkoani Arusha.

Wakulima wa zao la nyanya watakiwa kupatiwa elimu sahihi ya zao hilo

Na Mwandishi wetu,TimesMajira,Online

MKUFUNZI wa zana za Kilimo kutoka Mamlaka ya Elimu na ufundi stadi VETA,Mhandisi Joseph Kimako amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha katika maeneo ya uzalishaji wa nyanya kujengwa viwanda vya usindikaji ili kuondoa hasara ya upotevu wa zao hilo.

Akitoa kauli hiyo jana mkoani Arusha wakati wa Mkutano wa 12 wa Kimataifa wa Taasisi ya wahandisi nchini uliofanyika Ngurudoto,Mhandisi Kimako amesema zao la nyanya ni moja kati ya zao muhimu linaloimarisha afya ya mlaji lakini pia kipato kwa wazalisha wadogo hapa nchini.

Amesema Mamlaka yao ilifanya tafiti ambayo ilijikita katika Mkoa wa Morogoro katika wilaya ya Kilosa na Mvomero maeneo ya Doma na Dumila kwa wakulima wa Nyanya ambapo waligundua kuna upotevu Mkubwa unatokea kwa wakulima wa nyanya kabla na baada ya kuvuna unaosababishwa na wakulima kutopata elimu Sahihi ya zao la nyanya.

Mhandisi Kimako amesema kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha wakulima hao wanapatiwa elimu juu ya uvunaji wa nyanya ili kupunguza hasara wanazozipata.

“Kama kukiwepo kwa viwanda vya usindikaji,wakulima wakapewa elimu juu ya uvunaji huku kalenda za mazao za kilimo zinafatwa kwa uhakika ili wakulima walime zao hili kulingana na msimu mzuri wa soko la nyanya litasaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia upotevu wa zao hilo,”amesema na kuongeza

“Sisi kama VETA tutaendelea kuwasaidia wakulima kwa kuwashauri namna bora ya kupunguza hasara ya upotevu wa zao za nyanya kabla na baada ya kuvunwa kwa kuhakikisha tunawapa elimu na kuwasaidia katika kuwaongoza katika ulimaji wao,”amesema Mhandisi Kimako