Na Esther Macha,TimesMajira Online, Mbeya
MBUNGE wa Jimbo Mbeya ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amewaomba wananchi wanaoishi jirani na vyanzo vya maji kuwa mabalozi wazuri wa kutunza vyanzo vya maji ili watu wengine waendelee kuhudumiwa .
Dkt .Tulia amesema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mradi wa maji katika kata ya Itende Jijini hapa ambapo amesema kuwa vyanzo vya maji vilivyotembelewa vipo vizuri hivyo wananchi waendelee kutunza vyanzo hivyo ili huduma hiyo iendelee kutolewa kwa wananchi wa maeneo mengine .
“Naomba ndugu zangu kwa kushirikiana na Mamlaka ya maji tusaidiane kutunza vyazo vya maji tunaposherekea uzinduzi wa mradi huu basi twende kwa pamoja kwenda kutunza vyanzo vyetu vya maji ili maji yaweze kupatikana kwa wingi na serikali yetu itaweza kutuhudumia kama vyanzo vya maji vipo na tutaweza kutengeneza miundo mbinu vizuri “, amesema Dkt. Tulia.
Aidha Dkt. Tulia amesema baadhi ya sehemu zenye vyanzo vya maji vimekatwa miti hali ambayo inaweza kuleta changamoto ya upatikanaji wa maji miaka ya baadaye hivyo wananchi mnapaswa kutunza vyanzo vya maji ili watu wengine waweze kupata huduma hiyo.
Akizungumzia ulipaji wa bili za maji Dkt.Tulia amewataka wananchi wa kata ya Itende kuonyesha mfano wa kulipa bili za maji kwa wakati ili wananchi wengine waweze kufikishiwa huduma kwa wakati .
Hata hivyo Dkt. Tulia amesema kuwa haitakuwa vizuri mwanamke atuliwe ndoo kichwani alafu aje kukatiwa maji ,kwasababu ya madeni kuzidi.
“Tunataka mwanamke aendelee kufanya shughuli zingine za uzalishaji mali badala ya kwenda kutafuta maji umbali mrefu hivyo niwaombe mkawe mabalozi wazuri wa kulipa bili za maji ili huduma hii ya maji muendelee kuipata, ” amesema Mbunge huyo.
Akitoa taarifa ya Mamlaka ya Maji, Mkurugenzi Mtendaji wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya, Ndele Mengo amesema, hadi mwezi Septemba 2020 kulikuwa na wateja 69,832 na maunganisho hayo yanahudumia wakazi wapatao laki sita ambayo ni sawa na asilimia 76 ya wakazi wanaoishi kwenye mtandao wa majisafi.
Aidha Mengo amesema katika kuhakikisha watu wote wanapata huduma muhimu ya majisafi mamlaka imekuwa ikifanyia utafiti na hatimaye kuwapatia maji bure wananchi ambao huonekana hawana uwezo wa kulipia huduma ya maji na kwamba jumla ya wateja wasiojiweza 87 wanapata huduma ya maji bure kiasi cha uniti tano kila mwezi.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi