October 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ushindi mechi Azam, Yanga kuamua mbabe

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) Azam FC leo watakuwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Azam Complex kuwakaribisha Yanga ambao wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu.

Leo Novemba 25 timu hizo zinakutana katika mchezo wao wa 25 na ambao unatarajiwa kuwa miongoni mwa mechi bora msimu huu kutokana na ubora wa vikosi vya timu zote mbili ambazo zipo kwenye nafasi ya kuwania ubingwa wa Ligi wa msimu huu.

Lakini pia timu hizo mbili zimejikusanyia alama 25 kila moja zikitofautiana idadi ya magoli ya kufunga na kufungwa.

Katika mechi zao 24 zilizopita, hadi sasa ameshindwa kupatikana mbabe kwani kila mmoja amemfunga mwenzake mechi nane na zimetoka sare katika michezo nane hivyo atakayemfunga mwenzake katika mchezo wa leo basi atakuwa mbabe.

Kingine kinachotajwa kuleta ugumu katika mchezo huo ni matokeo ya kila mmoja katika mechi zao zilizopita kwa Azam ataingia na kumbukumbu mbaya ya kutoka kufungwa goli 1-0 na KMC huku Yanga ikilazimishwa sare ya goli 1-1 na Namungo.

Akizungumza kuelekea kwenye mchezo huo, kocha msaidizi wa Azam FC, Bahati Vivier amesema kuwa, licha ya kuwa wapinzani wao wanahistoria kubwa lakini wataziweka pembeni na kuangalia dakika 90 zitaamua vipi.

Amesema, wana imani kubwa vijana wao watafanya vizuri katika mchezo huo
na kuendelea kuiweka timu yao kwenye uongozi wa Ligi kwani tayari wameshafanyia kazi kilichowakwamisha kwa KMC.

Bahati amesema kuwa, kikosi chao cha leo kitakuwa na mabadiliko kwani wachezaji wa kikosi cha kwanza ambao walikuwa kwenye majukumu ya timu zao za Taifa wamesharejea kikosini jambo litakaloongeza morali ya kusaka ushindi.

“Ushindi wa leo utatuweka kwenye nafasi nzuri zaidi katika mbio za ubingwa msimu huu hivyo nina imani wachezaji wetu watapambana na kupata alama tatu muhimu na jambo zuri ni kuwa hakuna mwenye presha itakayoweza kutugharimu kwani tumeshazungumza na tunaamini leo ni siku yetu,” amesema kocha huyo.

Nahodha ya kikosi hicho, Agrey Moris ameweka wazi kuwa wanajua kuwa mchezo wa leo utakuwa mgumu na wanaelewa uwezo walionao wapinzani wao lakini wao watakuwa na faida zaidi kwani watakuwa katika uwanja wa nyumbani waliouzoea.

Amesema kuwa, timu yoyote itakayojituma na kuchukua alama tatu basi itakuwa imejiweka kwenye nafasi nzuri ya kuwania ubingwa msimu huu hivyo hawawezi kuiachia nafasi hiyo iwapite.

“Msimu huu Ligi ni ngumu na ukiangalia timu tatu za juu zote zinawania nafasi ya kiutwaa ubingwa hivyo tunatambua kuwa mchezo utakuwa mgumu na ndio maana tumejipanga kucheza kwa utulivu katika uwanja wetu wa nyumbani ili kuchukua alama zote tatu na kila mchezaji atajitoa kwa asilimia 100, ” amesema Moris.

Kwa upande wake Afisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz amesema kuwa, hasira walizoshindwa kuzimaliza kwa Namungo watakwenda kuzimaliza leo katika mchezo wao dhidi ya Azam.

Amesema, tayari kocha Cedric Kaze ameshafanyia kazi makosa aliyoyaona kwenye mchezo wao uliopita na amewapa mbuni bora ambazo zitawafanya wachezaji wao kuchukua alama tatu.

“Hatutajali kuwa tupo ugenini kwani tunachokihitaji ni alama tatu, tunaamini kuwa wachezaji wetu wataweza kuandika historia nyingine katika uwanja wa Azam licha ya kuwa mechi hizi haziamuliwi na historia,” amesema Nugaz.