November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ufaransa yatenga euro Mil. 120 kushughulikia usawa wa kijinsia

Na David John, TimesMajira online

BALOZI wa Ufaransa nchini Tanzania Fr’ed’eric Clavier amesema, nchi yake imetenga fedha kiasi cha euro milioni 120 kushughulikia usawa wa kijinsia kupitia Mashirika na Asasi za kiraia kwa miaka 5 ijayo kwenye miradi inayolenga masuala ya jinsia ulimwenguni kote.

Amesema, kwa Tanzania itafadhili miradi 2 ya kuwawezesha wanawake ili kuweza kuzalisha 50% ya chakula na kuimarisha uwezo wa wanawake kwa kuwasaidia kupitia uwezeshwaji wenye thamani ya euro milioni 1.5 katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Clavier ameyasema haya Jijini Dar es Salaam katika mkutano wao na Waandishi wa habari ambapo pia mabalozi na wawakilishi kutoka mataifa mengine ya ulaya walihudhulia na ajenda kubwa ilikuwa ni uwepo wa siku 16 za kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake

Akizungumzia hilo, Balozi Clavier amesema kupingana na Ukatili wa Kijinsia ni swala lenye kipaumbele kikubwa na linahitaji kuangaliwa kwa karibu kwa kushirikiana na serikali na Taasisi zingine zikiwepo Asasi za kiraia na Mashirika ya UN.

“Siku 16 za uanaharakati dhidi ya ukatili wa kijinsia ni kampeni muhimu za kumulika Ukatili wa Kijinsia na kufanya kazi pamoja ili kuleta mabadiliko ya tabia wakiwemo wanaume,” amesema Balozi Clavier.

Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Manfredo Fanti na mabalozi wengine wanachama wa Umoja huo wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania wakishirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la (UN Women) na Mashirika yasiyo ya Kiserikali (NGO’s) kwa pamoja wamezungumzia kuzinduliwa kwa Kampeni hiyo maalum ya siku 16 yenye lengo la kupinga ukatili wa Kijinsia dhidi ya Wanawake.

Akifafanua zaidi, mwakilishi Mkazi wa Shirika la UN Women Tanzania Ms.
Lianne Houben amesema, katika siku 16 za kupinga ukatili na unyanyasaji dhidi ya wanawake kuazia Novemba 25 hadi Desemba 10,2020 wameandaa shughuli mbalimbali zitakazofanyika Dar es salaam na maeneo ya pembezoni ukiwemo mkoa wa pwani ili kuweza kuifikia jamii tofauti na kuweza kupeleka kile walichokiandaa.

“Ujumbe muhimu wa Umoja wa Ulaya na nchi zingine wanachama kwa mwaka huu ni Maendeleo ya Mwanamke ni faida kwa Jamii Nzima ambayo imeunganishwa kwa karibu na kauli mbiu ya taifa la Tanzania ya 2020, isemayo Tupinge Ukatili wa Kijinsia. Mabadiliko yanaanza na Mimi,” amesema Houben.

Amesema, Lengo kuu la mwaka huu ni kukuza uelewa wa watoto juu ya upungufu wa kuondoa Ukatili wa Kijinsia kupitia uwezeshaji wa wanawake kiuchumi huku maadhimisho ya mwaka huu yakiwa na washiriki kutoka katika Taasisi za kijamii (TACCI), Jukwaa la Heshima la Watoto (CDF).

Pia watakuwepo watu mashuhuri kama vile Millad Ayo, Idris sultan, Dina Marios, Dkt.kumbuka na Dida Shaibu pamoja na Wasanii wa Uchoraji na wafanyabiashara wachanga wa kike pia wametajwa kushiriki.

Katika kukamilisha siku hizo 16 ujumbe wa Umoja wa ulaya, Ubalozi wa Ufaransa, Ujerumani na Ubelgiji watafanya tukio la kuhamasisha Umma chini ya kaulimbiu “usiku wa Wanawake kuwezeshwa”.

“Lengo la hafla hii ni kutengeneza nafasi ambayo itamwezesha Mwanamke wa Kitanzania kuweza kujieleza sambamba na maonyesho ya msanii wa kike pamoja na mawasilisho mafupi kutoka kwa wanawake wanaoanza.

Katika mkutano huo pia balozi wa ujerumani.na Netherland,pamoja na wengineo walizungumzia tukio hilo muhimu la kupinga unyanyasaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na kwanamna nchi zao zinavyokabiliana na changamoto hiyo.