November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania nje ya nchi washauriwa kununua hisa kwa kutumia simu

Na Jackilne Martin, TimesMajira Online, DSM

WATANZANIA wanaoishi nje ya nchi (diaspora) na wale walioko mbali na masoko ya hisa wamehimizwa kuwekeza nchini kupitia soko la hisa mitaji kwa kutumia mfumo wa kuuza na kununua hisa kwa teknolojia ya simu mkononi.

Wito huo umetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama alipokutana na waandishi wa habari wakati alipokuwa akizindua mfumo wa uuzaji na ununuzi wa hisa kwa kutumia simu za mkononi, mfumo ambao unaojulikana kama Hisa Kiganjani.

Mkama amelitaka Soko la Hisa na wadau wote kuhakikisha kuwa mfumo wa kuuza na kununua hisa kwa njia ya simu za mkononi unasaidia kuwezesha Watanzania waliopo nje ya nchi kushiriki katika uwekezaji nchini kwa kuwa mfumo huo utaleta matokeo chanya katika kujenga sekta jumuishi ya fedha.

Mkama amesema “Kwa mujibu wa utafiti wa Finscope Tanzania wa mwaka 2017 zaidi ya asilimia 60 ya watu wazima wanatumia huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi, hivyo uwepo wa mfumo wa kutumia simu za mkononi utaleta matokeo chanya katika kujenga sekta jumuishi ya fedha”.

Aidha amesema takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) za kipindi cha robo mwaka kilichoishia Septemba 2020, idadi ya watumia huduma za fedha nchini kwa njia ya simu ni milioni 49.2 huku.

Mkama ameongeza kuwa mfumo wa Hisa Kiganjani utasaidia kuongezeka kwa miamala na mchango katika jitihada za kuongeza uelewa na elimu ya fedha kwa Umma;

“Uuzaji na ununuzi wa aina hii kwa kutumia simu ya mkononi utaongeza miamala katika soko la hisa na hivyo ukwasi wa soko la hisa utaongezeka, Hisa kiganjani itaongeza mchango katika jitihada za kuongeza uelewa na elimu ya fedha kwa umma, jitihada zinazofanywa na DSE na CMSA” amesema Mkama.

Mkama ametoa wito kwa uongozi wa soko la hisa la Dar es Salaam na kampuni zote zenye leseni kutoka mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana kuhamasisha matumizi ya mfumo huu wa Hisa kiganjani ikiwa ni pamoja na kuingiza elimu ya matumizi yake kwenye mipango yao ya kila mwaka ya elimu kwa umma.