October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Nchi zapambana kushiriki Karate Afrika Mashariki

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KATIBU mkuu wa Chama cha Mchezo wa Karate Tanzania, Sensei-Jerome Mhagama amesema
bado nchi mbalimbali za ukanda huu wa Afrika Mashariki zinapambana kupata vibali ya Covid-19 ili kuweza kuthibitisha ushiriki wao katika mashindano ya mchezo wa Karate ya Afrika Mashariki ‘East African Shotokan Karate Championship’ yatakayofanyika mwezi ujao.

Tanzania itakuwa mwenyeji wa mashindano hayo ambayo yameandaliwa na klabu ya Serengeti kwa kushirikiana na chama hicho yakiwa na lengo la kuimarisha ujirani mwema na kuhamasisha watu kurudi michezoni baada ya shughuli hizo kusimama kwa muda mrefu kutokana na janga la mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19.

Mbali na kuhamasisha watu kurudi michezoni lakini pia mashindano hayo yatakuwa na ushindani baina ya timu moja na nyingine, kwani yatakuwa ya mtu mmoja mmoja ‘Open Championship’ ambayo pia itashirikisha washiriki kutoka nchi zitakazoshiriki.

Katika mashindano hayo, Tanzania itawakilisha na klabu mbalimbali ambazo kwa sasa zinaendelea na mazoezi ili kuhakikisha kuwa zinafanya vizuri katika mashindano hayo.

Sensei Jerome amesema, hadi sasa timu zilizothibitishani ni zilezi za Rwanda, Burundi, Kenya huku wakiendelea kusubiri kuona kama nchi nyingine zitaweza kuthibitisha kabla ya Desemba 13 ambapo ndipo watakapofunga mchakato huo.

Amesema, kilichopelekea nchi hizo kuchelewa kuthibitisha hadi sasa ni jitihada wanazoendelea kuzifanya za kufuatilia vibali vya ruhusa ya kusafiri kutokana na mipaka yao kuendelea kufungwa kutokana na kuendelea kukabiliwa na Covid-19.

“Tunaendelea kusubiri na kuzipa muda wa kuthibitisha ushiriki wao nchi ambazo bado zinaendelea kupambana kusaka vibali, tunatambua kuwa vyama husika vinaendelea na jitihada za kufuatilia vibali kutokana na mipaka ya nchi zao kuendelea kufungwa kutokana na Covid-19 hivyo tutavuta subira hadi Desemba 13 ambapo ndipo tutafunga rasmi mchakato huu, ” amesema Sensei Jerome.

Akizungumzia maandalizi kiongozi huyo amesema kuwa, hadi sasa maandalizi yote yanaendelea vizuri na wao kama chama wanashirikiana bega kwa bega na klabu ya Serengeti pamoja na kuzipongeza klabu ya mchezo wa karate ambazo zimekuwa zikisaidia katika maandalizi kuelekea mashindano hayo.

“Safari hii klabu ya Serengeti imesaidiana na Chama chetu kuandaa mashindano haya na tunaimani kubwa kuwa tutafikia na kuwa sana na klabu za kimataifa ambazo zimejitanua na kutengeneza kalenda zao za mwaka hivyo tunawapongeza sana klabu hii na hadi sasa maandalizi yanaendelea vizuri, ” amesema Jorome.

Mashindano hayo pia yatatumika kama sehemu ya maandalizi na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ambayo ilipata mwaliko ya kwenda kushiriki mashindano ya ya 15 ya Dunia ya mchezo wa Karate ‘Funakoshi Gichin Cup 15th Karate World Championship Tournament’ yanayofanyika kila mwaka.

Mwaliko huo ulikuwa ni heshima kubwa kwa Tanzania ambayo ni nchi pekee katika ukanda huu wa Afrika Mashabariki kuupata kwa mara ya pili baada ya ule wa kwanza walioupata mwaka 2014 ambapo ilishiriki bila kupeleka jaji.

Mbali ya kupata nafasi ya kushiriki mashindano lakini pia mwaliko uliotolewa uliipa Tanzania nafasi ya kipekee kwa kutoa Jaji wa michuano hiyo ambaye ni Sensei Jerome Mhagama.

Katika mashindano ya kwanza yaliyofanyika nchini Thailand, Jerome alishiriki kama mchezaji na kupata uzoefu huku mara ya pili mwaka 2014, Tanzania ilipata nafasi ya kutoa jaji na kufanikiwa tena kuiwakilisha nchi.

Wakiwa katika maandaalizi kujiweka sawa na mashindano hayo, yalilazimika kuahirishwa hadi mwakani kutokana na mlipuko wa Covid-19 hali iliyopelekea mipaka ya nchi nyingi kufungwa.