October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watanzania watakiwa kujenga tabia ya kuandika wosia

Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

WITO umetolewa kwa wananchi kujenga tabia ya kuandika wosia na kuachana na dhana potofu  ya kwamba  kuandika wosia ni unajitabiria kifo.

Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea wa Tanganyika(TLS) Mwanza Chapter Wakili Lenin Njau kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria yanayofanyika Jijini Mwanza kuanzi Novemba 12 hadi 18 mwaka huu ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni usimamizi bora wa mirathi kwa maendeleo ya familia ambayo imebeba ujumbe unaogusa maisha ya jamii ya kila siku. Picha na Judith Ferdinand

Wito umetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea wa Tanganyika (TLS), Tawi la Mwanza, Wakili Lenin Njau katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria yanayofanyika Jijini Mwanza ambayo yalianza Novemba 12 hadi 18 mwaka huu.

Katika maadhimisho hayo yenye kauli mbiu ya ‘Usimamizi Bora wa Mirathi kwa Maendeleo ya Familia’ yamebeba ujumbe unaogusa maisha ya jamii ya kila siku.

Wakili  Njau amesema mara nyingi tatizo la mirathi huwa kubwa endapo marehemu hajaacha wosia wowote na kuzitaja baadhi ya faida za wosia ni pamoja na anayeandika kuamua kwa hiari yake mali zake ziende kwa nani, badala ya kuacha jukumu hilo kwa msimamizi wa mirathi ambaye anaweza kugawa kinyume na ambavyo angetaka mwenyewe, hivyo kusababisha dhuluma kwa familia au walengwa halali walioachwa hapa duniani.

“Napenda kutoa wito kwa watu wote wanawake na wanaume kwani imejengeka dhana potofu kuwa mara nyingi wanaume ndio hufa kwanza kabla ya wake zao na hivyo wanawake wengi kuwahimiza wanaume wao kuandika wosia na wao kujisahau, tuachane na dhana potofu kuwa kuandika wosia eti ni kujitabiria kifo, hii sio kweli kwani kifo kipo tu hakuna mantiki yoyote endapo tutatumia nguvu kubwa kwa kufanya kazi kwa bidii na kutafuta mali halafu ushindwe kuacha wosia wa namna gani ungependa mali hizo zigawanywe pindi unapofariki,” amesema Wakili Njau.

Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za wanawake na wasichana la Kivulini Yassin Alli akizungumza na waandishi wa Habari kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya msaada wa kisheria yanayofanyika Jijini Mwanza kuanzi Novemba 12 hadi 18 mwaka huu ambapo kauli mbiu ya maadhimisho hayo ni usimamizi bora wa mirathi kwa maendeleo ya familia ambayo imebeba ujumbe unaogusa maisha ya jamii ya kila siku. Picha na Judith Ferdinand

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema suala la mirathi linamgusa kila mtu moja kwa moja na ndio sababu wanazungumzia umuhimu wake katika maadhimisho hayo kwa mwaka huu huku wanawake wamekuwa wahanga wakubwa inapofika katika kufuatilia mirathi hasa baada ya kuondokewa na wenzi wao.

Mongella ametoa wito wa kuendelea kujenga tabia ya kufuatilia na kupata elimu na msaada wa kisheria, kuendelea kuwatumia wadau mbalimbali ambao wanatoa msaada huo katika jamii huku serikali ikiunga mkono jitihada mbalimbali zinazoendelea kuhakikisha wananchi wanapata elimu na ufahamu juu ya suala hilo na kuzitaka asasi za kirai ziwafuate wananchi walipo ili kuwahudumia.

Naye Mkurugenzi wa Shirika la kutetea haki za wanawake na wasichana la Kivulini Yassin Alli, amesema kumekuwa na changamoto ya mjane ama mtoto wa marehemu ambaye alikuwa ameajiriwa sehemu fulani kuombwa barua kuthibitishwa kazini, banki statemate ( taarifa za kibenki) ambayo yeye sio mhusika pamoja na  hati ya malipo ya mshahara ya miezi mitatu na kitambulisho cha NIDA hali inayokwamisha masuala ya mirathi hivyo aliomba kuondokewa kwa vikwazo hivyo.