Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online
MSAFARA wa viongozi na wachezaji wa timu ya mpira wa kikapu ya jijini Mwanza leo usiku umefika Jijini Dodoma tayari kwa ajili ya mashindano ya mpira wa kikapu ya CRDB Bank Taifa Cup yatakayoanza kutimua vumbi kesho Novemba 13 katika Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma.
Mwanza wataingia katika mashindano hayo huku wakiwatangaza hali ya hatari kwa wapinzani wao kwani msimu huu wamepania kunyakua ubingwa wa mashindano hayo baada ya kushindwa kufanya hivyo misimu mitatu mfululizo baada ya kumaliza katika nafasi ya pili.
Kocha mkuu wa timu hiyo Benson Nyasebwa ameuambia Mtandao huu kuwa, wamejiandaa vilivyo kuhakikisha wanatimiza mipango yao ya kuchukua ubingwa safari ambayo waliianza muda mrefu.
Amesema kuwa, safari hii katika mashindano hayo, kauli mbiu yao itakuwa ni ‘Motion, Offen’ pamoja na kulinda na kukaba kwa nafasi ‘Defence zone half man to man’ ambazo wanaamini wakizitendea haki ipasavyo basi kazi itakuwa rahisi kwao.
Licha ya kuwakosa nyota wake wawili Shaaban Ally ambaye ni MVP wa Mwanza na Moses Jackson lakini hana wasiwasi kwani bado ana wachezaji wengi wazuri ambao watampa kile anachokihitaji.
“Mashindano ya Taifa Cup ya msimu huu ni muhimu sana kwetu na ndio maana tulianza maandalizi mapema ambayo yametujenga kwa ajili ya ushindani, mipango yetu ni kuhakikisha tunarudi Mwanza na ubingwa na tutahakikisha tunalitekeleza jambo hilo,” amesema kocha benson.
Katibu wa timu hiyo, Shomary Almas amesema kuwa, msafara wao umejumuisha wachezaji 20 wanaounda timu ya wanawake na wanaume pamoja na viongozi wanne.
Kiongozi huyo amesema kuwa, hawana wasiwasi kwenye mashindano hayo ya mwaka huu kwani walifanya maandalizi ya kutosha ili kuwa bora kwani uzuri walishajua wanakosea wapi na kupafanyia kazi ili kuhakikisha msimu huu wanatwaa ubingwa huo.
Wakati wanajiandaa na mashindano hayo, Kamishna wa Mashindano na Ufundi wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Mwanza, Haidari Abdul aliuambia Mtandao huu kuwa, kutokana na umuhimu wa mashindano hayo, waliamua kusitisha kila kitu ikiwemo mechi za fainali za Ligi ya Mkoa MRBA ambazo sasa zitachezwa mara tu baada ya kumalizika kwa mashindano hayo.
Amesema kuwa, safari hii wamepania kutwaa ubingwa na ni lazima tukalitimize hilo na ndio maana walichagua wachezaji bora ambao wanaamini wataweza kuwpa matokeo wanayoyataka.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025