November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Riadha Singida wapata viongozi wapya

Na Damiano Mkumbo, TimesMajira Online, Singida

CHAMA cha mchezo wa Riadha Mkoa wa Singida kimepata viongozi wake wapya watakaokiongoza katika kipindi cha miaka minne ijayo.

Viongozi hao wamepatikana katika uchaguzi ulioambatana na Mkutano Mkuu uliyofanyika mwishoni mwa wiki ambapo aliyekuwa Katibu Msaidizi wa chama hicho, Juma Mataka amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya baada ya kupata kura 16 kati ya 22 zilizopiagwa na kuwashinda wenzake wawili.

Akitangaza matokeo baada ya zoezi hilo kukamilika kwenye ukumbi ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Mjini hapa, msimamizi wa uchaguzi huo, Henery Kapela amesema kuwa, wagombea wengine katika nafasi hiyo walikuwa ni pamoja na aliye maliza muda wake Rashid Itembe aliyepata kura 5 na Ally Jumbe aliyeambulia kura moja.

Kapela ambaye ni Afisa Michezo wa Mkoa amewataja wengine kuwa ni Makamu Mwenyekiti, Said Swalehe aliyepita kwa kura 22 za ndiyo, Katibu Mtendaji ni Joel Ngingo aliyepata kura 13 na kumshinda Beno Msanga aliyekuwa akitetea nafasi yake ambaye alipata kura 9 huku Meshack Matandala akipata ujumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Riadha wa Taifa.

Nafasi ya Katibu msaidizi imechukuliwa na James Mkoka, Mweka hazina ni Efrasia Mtinangi, na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji imekwenda kwa Damiano Mkumbo aliyekuwa Mgombea pekee akiwa kura 20 za ndiyo na mbili za hapana huku nafasi mbili zilizo wazi zitajazwa baadaye.

Akizungumza baada ya kutangazwa na kufunga mkutano Mwenyekiti huyo mpya Juma Mataka amewashukuru wajumbe kwa kumpa kura nyingi na kuahidi kujenga ushirikiano na umoja katika kuleta mabadiliko ya mchezo huo Mkoani Singida na kuendelea kudumisha hadhi yake Kitaifa na Kimataifa.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Juma Kilimba ameeleza kuwa, watahakikisha wanaendelea kuuenzi uwanja wa michezo uliopo Mjini Singida unaomilikiwa na Chama hicho wa Leti ambao ulimepewa jina hilo kwa ajili ya kumwenzi Jemedari mwanamke wa kabila la Kinyaturu aliyepambana na wakoloni wa Kijeruman walipoingia Mkoa wa Singida.

Akitoa salamu wakati wa sherehe ya uzinduzi wa Kitabu kilicho andikwa na Msaidizi wa Askofu Dkt. Cyprian Hilinti cha Misemo na Methali za Kinyaturu ‘Fahamu Urithi na Utajiri Unaofifia’ iliyofanyika eneo la kanisa hilo, Kilimba pia amemshukuru mwandishi huyo na kutoa wito watu wa Mkoa huo kupenda kuandika na kusoma mambo yanayohusu Utamaduni, Uchumi, Jamii, Michezo ili kuchochea mabadiliko katika maendeleo ya kisasa.