November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mo Noray azitaka Simba, Yanga kujijenga Kimataifa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

MDAU wa soka na Mkurugenzi wa Kampuni ya Ujenzi ya Tanzania Building Works LTD, Mohamed Noray amezitaka klabu za Simba na Yanga kujijenga Kimataifa ili ziweze kufanya vizuri pindi zinaposhiriki michuano ya Kimataifa Barani Afrika.

Noray ambaye Kampuni yake ndio inakarabati Uwanja wa Ndani wa Taifa (Indoor Stadium) unaotumika kwa ajili ya michezo mbalimbali ikiwemo ngumi, Mpira wa Kikapu, Netiboli na mingine ili kufanikisha mambo yanakwenda sawa kwenye michezo baada ya kuona sekta hiyo inakua kwa kasi.

Akizungumza na Mtandao huu Noray amesema, timu hizo zinatakiwa kujijenga vizuri kuhakikisha zinafanya vyema kwenye michuano ya Kimataifa.

“Ki ukweli nimelishuhudia pambano leo ambalo lilikua la kuvutia huku kila timu ikionesha kandanda safi, najua Simba inashiriki Ligi ya Mabingwa barani Afrika hivyo ni vyema ikakiandaa kikosi chake vizuri ili kuweza kupambana kuhakikisha inafika hatua nzuri na hata kunyakuwa ubingwa kama zilivyo klabu za TP Mazembe na zinginezo Afrika ambao wamekuwa wakifanya vema kwenye mashindano hayo, ” amesema Noray.

Amesema, katika mchezo huo Yanga walionesha mchezo mzuri kipindi cha kwanza na kufanikiwa kupata goli kwa njia ya penalti baada ya beki wa Simba Joash Onyango kumchezea vibaya Tuisila Kisinda na Michael Sarpong aliweza kuipatia Yanga goli la kuongoza.

Amesema kuwa, kipindi cha pili Simba walionekana kulisakama kama nyuki lango la Yanga ambao walioamua kulilinda goli lao lakini kutokana na jitihada za timu hiyo walifanikiwa kusawazisha katika dakika ya 86 kupitia kwa beki wake Joash Onyango akiunganisha kwa kichwa mpira wa kona.

Mbali na timu hizo kutoshana nguvu pia, Noray ameitaka timu ya Taifa ya Tanzania Taifa Stars kufanya maandalizi ya kutosha ili iweze kufanya vizuri katika mchezo wake wa kufuzu Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), dhidi ya Tunisia utakaochezwa Novemba 13 mwaka huu nchini Tunisia.

“Mimi naitakia kila la kheri timu ya Taifa ya Tanzania iweze kufanya vyema katika mchezo wao wa Novemba 13 dhidi ya Tunisia, naamini kwa kikosi tulichokuwa nacho kikiongozwa na nahodha wake Mbwana Samatta anayekipigia nchini Uturuki nina imani tutapata matokeo mazuri,” amesema Noray.

Hata hivyo, mdau huyo wa soka amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli kwa kutolea macho suala la michezo ikiwemo viwanja kwa kuanza na ujenzi wa Uwanja wa mpira utakaoingiza watu laki moja Jijini Dodoma.

Noray amesema, kama Rais Magufuli anaona umuhimu wa michezo hawana budi kumuunga mkono, kwani sekta ya michezo ni sekta muhimu hivyo Watanzania watafarijika kuona rais akitolea macho sekta hiyo ambayo inapendwa na wengi.