Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Arusha
MWANAFUNZI wa kidato cha tano katika shule ya sekondari ya UWC East Africa ya jijini Arusha ,Aalaa Riyaz Somji ameibuka mshindi wa jumla katika mashindano ya Gofu ya ‘Diplomatic Golf 2020’ yaliyofanyika katika uwanja wa Kili Golf uliopo Usa River Arusha.
Mbali na ushindi huo Aala mwenye umri wa miaka 17 pia ameibuka mshindi wa kwanza wa mchezo huo kwa upande wa wanawake huku akijinyakulia zawadi ya saa pamoja na mapumziko ya siku tatu katika Hoteli ya Manta Resort pamoja na kulala usiku mmoja kwenye chumba kilichopo chini ya bahari.
Ikiwa ni mara ya pili kufanyika kwa mashindano hayo ya Diplomatic Golf 2020 yaliyodhaminiwa na Benki ya CRDB, yameshirikisha washiriki zaidi ya 150 kutoka mataifa 19 yakilenga kuwakutanisha wanadiplomasia, watendaji wakuu wa makampuni, wafanyabiashara wakubwa na wachezaji mbalimbali wa gofu ambao hawashiriki mashindano ya kitaifa na kimataifa.
Kwa upande wa wanaume mshindi wa kwanza ni Tender Singh Bansal aliyejinyakulia kiasi cha sh. milioni 1 fedha ambazo hata hivyo alizitoa kwa taasisi isiyo ya kiserikali ya SIMO ya Songea kwa ajili ya kusaidia watoto waishio kwenye mazingira magumu .
Akizungumza mara baada ya kukabidhi zawadi kwa washindi, mgeni rasmi katika mashindano hayo aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya nje ya nchi Damas Ndumbaro amesema kuwa, mashindano hayo yametumika katika kutekekleza diplomasia ya kiuchumi kwa vitendo.
“Tumekutanisha makundo yote haya pamoja wacheze mpira wa Gofu wafurahi ,lakini muhimu zaidi waongee masuala ya ushirikianao wa kiuchumi yaani kupitia mashindano kama haya tunatekeleza Diplomasia ya kiuchumi kwa vitendo , ” amesema Ndumbaro.
Amesema kuwa, kutokana na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika mashindano ya mwaka huu akatangaza rasmi uwanja wa Gofu wa Kili Golf uliopo Usa River jijini Arusha kuwa nyumbani mwa mashindano ya “Diplomatic Golf” na kwamba mwakani pia yatafanyika katika viwanja hivyo.
“Sasa naweza kutangaza rasmi kwamba ‘Kili Golf is a home of Diplomatic Golf’, tutakuwa na siku mbili na hii ni baada ya kukataa maombi ya washiriki wengine kutokana na idadi ya wachezaji tuliyokuwa tumejiwekea,” amesema Ndumbaro.
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma ya Prmier, Gibson Mlaseko amesema, CRDB wataendelea kusaidia michezo mbalimbali kwa kuwa ni sehemu ya jamii na inawezesha mashirikiano na kuboresha mahusiano baina yao.
“Gofu inatazamwa kama ni mchezo wa watu matajari peke yake lakini sisi kama CRDB tunaendelea kuwaalika na watu wengine kushiriki katika mchezo huu lakini pia kama CRDB tumeweka nguvu yetu katika mashindano haya kwa sababu seheumu ya mapato yanayopatikana katika tukio hili yanaenda kusaidia sehemu ya jamii ya watoto huko Songea, ”.
“tumeona ni jambo zuri kuwa sehemu ya msaada kwa jamii hii lakini pia tumetoa zawadi kwa wachezaji wawili walioweza kufanya vizuri katika mashindano haya hadi kiasi cha sh milioni moja fedha ambazo wameomba ziende kutumika usaidia watoto huko Songea,” ameongeza Gibson.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025