October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uzazi holela wakithiri Ilemela, waomba elimu ili kudhibiti

Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

Wananchi wa Mtaa na Mwalo wa Butuja Wilayani Ilemela Mkoani Mwanza wameiomba Serikali kupitia wataalamu wa afya kutoa elimu ya uzazi wa mpango kuanzia jamii ya watu wenye hali ya chini ikiwemo ya wavuvi.

Mmoja wa wananchi wanaoishi katika mtaa huo Esther Steven (BOFYA KUTAZAMA VIDEO) ambaye ni mama wa watoto wawili huku akiwa na ujauzito, amesema elimu kuhusu uzazi wa mpango wengi hawana uelewa huo hususani walio katika maeneo ya mialo ndio maana wanazaliana kwa wingi zaidi.

“Mimi elimu ya afya ya uzazi wa mpango nimeipata mara baada ya mwanagu wa pili kuumwa na kupewa rufaa ya kumpeleka Hospitali ya Bugando ndipo nilishauriwa kutumia njia ya uzazi wa mpango nikijifungua,” amesema Esther na kuogeza

kuwa bila kuifuata njia hiyo tunawaumiza watoto maana hawapati malezi bora na kuugua mara kwa mara kama mimi mwanagu wa kwanza ana miaka 3, wa pili mwaka 1 na nina mimba ambayo karibu nitajifungua hivyo tabu ninayoipata katika kuwahudumia hawa watoto ni kubwa na huyu wa pili anaumwa ,”.

Kwa upande wake Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Butuja, Ally Mkama amesema watu wengi wanaoishi maeneo ya kando kando ya ziwa hali zao za kipato ni duni wengi wao wanaona ngono ni starehe hali inayosababisha mimba zisizotarajiwa hususani katika jamii ya wavuvi.

Mkama amesema, sababu nyingine ni elimu ya uzazi wa mpango kwa watu wenye kipato cha chini hususani jamii ya wavuvi bado haijawafikia vizuri.

Mkama ameitaka Serikali kutoa elimu ya uzazi wa mpango kwa wananchi wenye kipato cha chini ili iwafikie kwa usahihi na kutoa fursa ya watoto kupata malezi bora sanjari na kutoa ushauri wa kuacha ngono zembe ili waepuke na magonjwa mbalimbali yanayoweza kusababisha kupoteza nguvu kazi ya taifa.