October 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Hassan Mwakinyo celebrates beating Sam Eggington in the second round of their Super-Welterweight contest at Arena Birmingham, Birmingham. (Photo by Nick Potts/PA Images via Getty Images)

Mwakinyo abadli ratiba ya mazoezi

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Dar es Salaam.

WAKATI bondia, Jose Carlos Paz kutoka Argentina anawasili leo mpinzani wake, Hassan Mwakinyo amebadili ratiba ya mazoezi na sasa anajifua saa nne kwa siku.

Mwakinyo ameweka kambi eneo la Magoroto, Muheza mkoani Tanga kuelekea pambano la kutetea ubingwa wa Mabara wa WBF na kuwania ubingwa mpya wa Mabara wa IBA wa uzito wa Super-Welter.

Bondia huyo anajifua chini ya Kocha, Hamis Mwakinyo pamoja na wasaidizi mbalimbali huku wakitumia video mbalimbali kumsoma Paz, ambaye ana rekodi nzuri.

“Nimehama nyumbani na kujichimbia huku, Magoroto kwa lengo la kufanya vyema katika pambano hilo, kujifua zaidi ya raundi 12 ili kupata stamina ya kwenda sambamba na mpinzani wangu,” amesema Mwakinyo.

Katika hatua nyingine, waandaaji wa pambano hilo wamesema tiketi kwa ajili ya pambano zitauzwa mtandaani kupitia Kampuni za Nilipe na Selcom.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Jackson Group Sports, Kelvin Twissa amesema viingilio kwa pambano hilo, vitaanzia sh 150,000 kwa eneo la kawaida na meza ya watu 10, itauzwa kwa sh. milioni tatu ambao watapata huduma mbalimbali zilizoandaliwa.

Twissa amesema mbali ya Mwakinyo na Paz, pia siku hiyo kutakuwa na mapambano makali ambapo bondia nyota wa kike, Zulfa Macho atazipiga na Alice Mbewe kutoka Zambia wakati Hussein Itaba atazichapa na Alex Kabangu katika uzito wa Super-Middle.

Siku hiyo pia bondia nyota kutoka Kenya, Fatuma Zarika atazichapa na Patience Mastara wa Zimbawe katika uzito wa Super Bantam.

Wakati huo huo, mpinzani wa Mwakinyo, Paz ameamua kuwasili mapema Tanzania ili kuzoea hali ya hewa.

Paz anatarajiwa kuwasili usiku saa 4.30 kwa ndege ya KLM na msafara wake utaambatana na kocha wake, Oscar Alberto Ramon.