Na Holiness Ulomi, TimesMajira Online
BAADA ya kukamilika kwa mashindano ya mpira wa kikapu ya Taifa (National Basketball League – NBL 2020), Chama cha Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) kimegeukia maandalizi
ya mashindano ya CRDB Taifa Cup yatakayoanza kutimua vumbi kuanzia Novemba 12 hadi 21 kwenye viwanja vya Chinangali.
Katika NBL, timu ya Kurasini Heats imefanikiwa kutwa taji hilo ambalo ni la pili msimu huu baada ya kuifunga Oilers kwa pointi 76-59 huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Don Bosco Panthers ya Dodoma ambao walifanikiwa kuifunga Vijana Basketball Club ya Dar es Salaam kwa pointi 80-77.
Kwa ushindi huo, bingwa Kurasini Heat itaiwakilisha Tanzania katika mashindano ya Kombe la Klabu Bingwa ya Afrika (Basketball Africa League – BAL) huku mshindi wa pili na wa tatu watawakilisha Tanzania katika mashindano ya klabu ya Kanda ya Tano ya Afrika (Zone V Club Championship /Challenge Cup).
Kwa upande wa wanawake bingwa JTK pamoja na mshindi wa pili wote watawakilisha Tanzania katika mashindano ya klabu ya wanawake ya Kanda ya Tano ya Afrika.
Akizungumza na Mtandao huu, Rais wa TBF, Phares Magesa amesema, maandalizi kuelekea mashindano hayo yanaendelea vizuri na timu zote zitakazoshiriki zipo kwenye maandalizi ya mwisho kabla ya kuanza rasmi kwa mashindano hayo.
Hadi sasa timu ambazo zitashiriki ni zile zile 36 za wanaume na wanawake kama ilivyotangazwa awali lakini pia mashindano hayo yatatanguliwa michuano ya timu za veterani za Benki ya CRDB, Bunge, Pazi, Bahari na timu za walemevu.
“Baada ya kumalizika kwa Ligi ya NBL na kupata wawakilishi katika mashindano ya kimataifa moja kwa moja tunaendelea na maandalizi ya michuano ya CRDB Taifa Cup ambayo itakwenda kuanza hivi karibuni na timu zote shiriki zipo kwenye maandalizi ya mwisho kuelekea mashindano hayo,” amesema Magesa.
More Stories
Samia awazawadi Stars milioni 700/-
Samia atoa bilioni 8/- kukarabati viwanja vya CHAN, AFCON
Rasmi Chatsoko mdhamini mkuu wa Goba Hills Marathon 2025