Na Joyce Kasiki, Dodoma


WADAU mbalimbali wa sekta ya afya wamejitokeza kushiriki maonyesho maalumu ya huduma na bidhaa za afya yanayofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea maadhimisho ya miaka 25 ya mwitikio dhidi ya UKIMWI Duniani yatakayofanyika Desemba Mosi mwaka huu.
Maadhimisho hayo yanafanyika mkoani Dodoma, huku maonyesho hayo yakilenga kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kinga, upimaji, matibabu na huduma mbalimbali zinazohusiana na maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU), magonjwa ya ngono na homa ya ini.
Akizungumza katika maonyesho hayo leo Novemba 29,2026, Afisa Huduma kwa Wateja Mwandamizi kutoka Bohari ya Dawa (MSD), Joan-Ruth Msangi, amesema taasisi hiyo inashiriki kwa kuonesha mchango wake katika upatikanaji na usambazaji wa bidhaa na vifaa tiba vinavyosaidia mapambano dhidi ya UKIMWI.
Amesema MSD ina jukumu la kununua, kuhifadhi, kusambaza na kuzalisha bidhaa za afya nchini, ambapo kwa sasa husambaza bidhaa hizo katika vituo 8,988 vya kutolea huduma za afya.

Ameeleza kuwa miongoni mwa bidhaa zinazotolewa ni kondomu za kiume na kike pamoja na vitendanishi vya kupima maambukizi ya VVU, vikiwemo vinavyomwezesha mtu kujipima mwenyewe.
Aidha, amesema MSD imeendelea kusambaza vifaa tiba mbalimbali vinavyotumika katika huduma za afya ya uzazi na matibabu kwa ujumla, ikiwemo vitanda vya kujifungulia, vitanda vya uchunguzi na taa za ukaguzi.
Kwa upande wake, Afisa wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI, Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP), Ester Ntulo, amesema mpango huo una jukumu la kuandaa sera na miongozo ya utoaji huduma, kuhakikisha upatikanaji wa vitendanishi na dawa pamoja na kusimamia ubora na mwendelezo wa huduma katika vituo vya afya.

Amesema kaulimbiu ya mwaka huu inasisitiza kuwa huduma bora za afya ni msingi katika kutokomeza UKIMWI, hivyo wananchi wanapaswa kutumia fursa ya maonyesho hayo kupata elimu na huduma zinazotolewa.
Ameongeza kuwa katika maonyesho hayo wananchi wanapata huduma za elimu na upimaji wa VVU, magonjwa ya ngono na homa ya ini, pamoja na huduma ya kujipima VVU kwa kuzingatia elimu na ushauri nasaha kabla ya upimaji.
Ntulo amewahimiza wakazi wa Dodoma na maeneo mengine kujitokeza katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete kuanzia Novemba 29 hadi Desemba Mosi, ambapo kutakuwa na huduma mbalimbali zikiwemo za magari maalumu yanayofika maeneo ya wananchi kutoa elimu na huduma za afya.
Naye Muelimishaji kuhusu masuala ya UKIMWI kutoka UNESCO, Rose John, ambaye pia ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. John’s, amesema kupitia maonyesho hayo wanatoa elimu kwa jamii kuhusu maambukizi ya VVU na umuhimu wa watu kufahamu hali zao za kiafya.

Amesema juhudi hizo zinaendana na malengo ya kimataifa ya 95-95-95, yanayolenga kuhakikisha asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wanajua hali zao, asilimia 95 ya waliogundulika kuwa na VVU wanapata matibabu na asilimia 95 ya wanaopata matibabu wanafikia kiwango cha virusi kisichoonekana kwenye damu.
Ameeleza kuwa elimu kuhusu VVU ni muhimu kwa jamii kuelewa njia za kujikinga, umuhimu wa kupima na namna ya kuendelea na maisha endapo mtu atagundulika kuwa na maambukizi.
Aidha, amesema mtu anapobainika kuwa na VVU hapaswi kukata tamaa, kwani kwa kutumia dawa za kurefusha maisha kwa usahihi na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya anaweza kuendelea na shughuli zake za kila siku.
Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuzingatia matumizi ya kinga, kupima kwa wakati na kuwa na mwenzi mmoja mwaminifu ambaye wamefahamu hali zao za kiafya, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kujikinga hata baada ya kupata majibu hasi.

More Stories
Tanzania,Nigeria kuandaa mkutano afya ya wanawake
Mchengerwa: Kila mgonjwa ahamasishwe kujiunga na bima ya afya
Wanafunzi wa DMI wang’ara Korea Kusini