November 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

AFERA-ARMFA yapitisha Azimio la Nairobi 

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Nairobi Kenya

CHAMA cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika (AFERA-ARMFA) kimepitisha Azimio la Nairobi kuhusu Mifuko ya Barabara ya Kizazi Kijacho, hatua inayolenga kuleta mageuzi  katika ugharamiaji na usimamizi wa miundombinu ya barabara barani humo.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha Mkutano Mkuu wa 23 wa Mwaka wa chama hicho uliofanyika  jijini Nairobi nchini Kenya,ambao uliokutanisha wenyeviti wa bodi, wakurugenzi wakuu wa mifuko ya barabara, mawaziri na wadau wa maendeleo, Rais wa AFERA-ARMFA, Mhandisi Rashid Kalimbaga, amesema,wakati umefika wa kubadilisha mijadala na tafiti zilizofanyika kuwa maamuzi ya kihistoria na utekelezaji wa vitendo.

“Katika siku hizi chache tumefanya kazi kubwa ya kujadili matumizi ya teknolojia (digitalisation), ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi na utawala bora wa shoroba za usafirishaji. Leo tumepiga hatua muhimu ya kugeuza kazi hiyo kuwa maamuzi thabiti,” amesema Mha.Kalimbaga.

Kwa mujibu wa Mhandisi Kalimbaga, Azimio hilo linazifunga nchi wanachama katika misingi mikuu yenye lengo la kuhakikisha uendelevu wa mifuko hiyo, ikiwemo kuwa na vyanzo vya mapato ya moja kwa moja, yanayotabirika na yanayoweza kuhimili mabadiliko ya nishati duniani.

Misingi mingine iliyopitishwa ni pamoja na kuwa na bodi zenye uwiano mzuri wa kiutendaji, kufanya maamuzi yanayozingatia takwimu sahihi, kutenga mifuko ya dharura kwa ajili ya majanga, kuingia mikataba ya utendaji kazi (performance agreements), kuongeza uwajibikaji kwa watumiaji wa barabara pamoja na usimamizi wa pamoja wa shoroba za kikanda.

Aidha, Azimio hilo limeweka ukomo wa muda ambapo kila mfuko mwanachama unatakiwa kuandaa mpango kazi wa kitaifa ndani ya kipindi cha miezi 12 na tathmini ya utekelezaji wake itafanyika katika Mkutano Mkuu ujao.

Vilevile, Mha.Kalimbaga amewahimiza wanachama wote kuendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za umoja huo kwa uwazi na kulipa ada zao za uanachama kwa wakati ili kuiwezesha sekretarieti kutekeleza mageuzi yanayokusudiwa.

Sanjari na hayo Mha.Kalimbaga ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Kenya, Wizara ya Barabara na Uchukuzi, pamoja na Bodi ya Barabara ya Kenya (KRB) kwa ukarimu wao wa hali ya juu uliowezesha kufanyika kwa mkutano huo kwa mafanikio makubwa.

Pia, amemshukuru Katibu Mtendaji wa AFERA-ARMFA na timu yake, Kamati ya Kisayansi, waongozaji wa mijadala, watoa mada pamoja na washirika wote wa maendeleo wakiwemo Umoja wa Ulaya (EU), SSATP na Kamisheni ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (ECA) kwa mchango wao uliowezesha mafanikio ya mkutano huo.