November 26, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanasheria Mkuu azindua mifumo ya kidijitali kuelekea dira 2050

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali,Hamza Johari amezindua Mifumo na Nyaraka mbalimbali zitakazotumika na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kipindi cha miaka mitano ijayo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amezindua nyaraka hizo na mifumo ya kidijitali katika hafla iliyofanyika Jijini Arusha.

Akizungumza katika uzinduzi huo,Johari amesema kuwa uwepo wa nyaraka na mifumo hiyo kutaimarisha na kuboresha utamaduni wa utendaji kazi ambao utaiwezesha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kutoa huduma bora zaidi na hivyo kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Johari amesema kuwa kupitia nyaraka na mifumo iliyozinduliwa, Ofisi itaelekeza nguvu kubwa katika kutoa huduma kinga za Kisheria “Preventive Legal Services” katika kuimarisha mapitio ya mikataba ya Kitaifa na Kimataifa kabla ya kusainiwa ili kubaini na kudhibiti mapema vihatarishi vya kisheria na kifedha.

“Tunazidi kuimarisha usimamizi wa majadiliano ya mikataba ili kuhakikisha masharti yake yanalinda maslahi ya Serikali na Taifa.” Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa uwepo wa nyaraka na mifumo hiyo utaiwezesha Ofisi kutoa mchango wake katika kufanikisha kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo, 2050.

Vilevile,Johari amesema kuwa Uzinduzi wa Nyaraka na mifumo hiyo una lengo la kuhakikisha kuwa Serikali inaendelea kutoa huduma za kisheria zenye ubora, maamuzi yanayozingatia sheria, mikataba inayolinda maslahi ya umma na mifumo madhubuti ya utatuzi wa migogoro inayochochea maendeleo endelevu ya Taifa la Tanzania.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Samwel Meneno akizungumza wakati wa kumkaribisha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesema kuwa nyaraka na mifumo iliyozinduliwa itaisaidia kuboresha utendaji kazi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hivyo kuiwezesha Serikali katika kutekeleza mipango ya maendeleo inayowekwa nchini.

Maneno ameeleza kuwa kuzinduliwa kwa nyaraka hizo ni kiashirio kwamba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imeanza utekelezaji rasmi wa Dira 2050.

Sambamba na uzinduzi wa Nyaraka na mifumo hiyo, hafla hiyo pia ilihusisha zoezi la utiaji saini wa Hati ya Makubaliano baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kwa ajili ya Ushirikiano wa Kitaalamu katika usimamizi wa Sekta ya Ununuzi wa Umma.

Hafla hiyo ya uzinduzi imehudhuriwa na Mhe. Balozi Prof. Dkt. Adelardus Lubango Kilangi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu na Balozi Prof. Kennedy Godfrey Gastorn, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu.

Hafla hiyo pia imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Makatibu na Manaibu Makatibu Wakuu wa Wizara, Wakuu wa Taasisi za Kisheria na Taasisi nyingine za Serikali.

Nyaraka na mifumo iliyozinduliwa katika hafla hiyo ni pamoja na Mpango Mkakati wake wa 2026/27–2030/31; Mkakati wa Mawasiliano wa 2026/27–2030/31; Mkataba wa Huduma kwa Wateja; Mfumo wa Maktaba ya Kielektroniki (e-Library); Mfumo wa Usimamizi wa Taarifa za Sekta ya Sheria (LSMIS); pamoja na Programu ya Maendeleo ya Rasilimali Watu na Mafunzo ya 2026/27–2030/31.