Na Joyce Kasiki,Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamure, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya UKIMWI Duniani yatakayofanyika mkoani humo Desemba 1, 2026, huku akisisitiza umuhimu wa jamii kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Virusi vya UKIMWI (VVU).
Senyamure ametoa wito huo jijini Dodoma wakati akizungumza kuhusu maandalizi ya maadhimisho hayo, akieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kinga, upimaji na matibabu ya VVU na UKIMWI.
Amesema maadhimisho hayo yanatarajiwa kufanyika Desemba 1, 2026, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Nchemba.
Amesisitiza kuwa maadhimisho hayo ni fursa muhimu ya kuwakumbuka watu waliopoteza maisha kutokana na UKIMWI, kuwafariji na kuwaunga mkono wanaoishi na VVU, pamoja na kutathmini hatua zilizofikiwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
āSerikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kinga, upimaji na matibabu ya VVU na UKIMWI,ā amesema Senyamure.
Aidha, ameitaka jamii kuendelea kushiriki katika mapambano hayo kwa kuzingatia elimu sahihi kuhusu VVU, kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi mapya na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya.
Katika maadhimisho hayo, wananchi watapata huduma mbalimbali za afya zikiwemo upimaji wa VVU, upimaji wa kisukari, uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi, ushauri nasaha pamoja na elimu ya afya.
Huduma hizo zinalenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu umuhimu wa kujua hali zao za kiafya, kupata ushauri na kuchukua hatua stahiki za kujikinga na magonjwa mbalimbali.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni āHuduma bora ndiyo msingi wa kukomesha UKIMWI,ā inayosisitiza umuhimu wa kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya, ikiwemo kinga, upimaji, matibabu na ufuatiliaji wa VVU.
Senyamure amewahimiza wananchi wa Dodoma na mikoa mingine nchini kutumia fursa hiyo kujitokeza kwa wingi katika maeneo yatakayotengwa kwa ajili ya maadhimisho hayo ili kupata huduma zinazotolewa bure au kwa utaratibu utakaowekwa na waandaaji.
Ameeleza kuwa mapambano dhidi ya UKIMWI yanahitaji ushirikiano wa jamii nzima, wakiwemo vijana, wazazi, viongozi na wadau wa afya, ili kuongeza uelewa na kupunguza maambukizi mapya.
Maadhimisho hayo pia yanatarajiwa kuhusisha utoaji wa elimu kwa vijana na wanafunzi, maonesho ya huduma za afya pamoja na shughuli mbalimbali za uhamasishaji zitakazolenga kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu VVU na UKIMWI.

More Stories
Makosa ya kibinadamu chanzo MV Mwanza kugonga mwamba
ARMFA yapokea programu ya kulinda mapato ya barabara
Vijana wahimizwa kutumia fursa za ubia miradi ya nishati