Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Kenya
ONGEZEKO la matumizi ya magari ya umeme barani Afrika linatarajiwa kuleta changamoto katika upatikanaji wa fedha za matengenezo ya barabara, hali iliyochochea Chama cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika (ARMFA) kupokea programu maalumu ya kukadiria athari za mabadiliko hayo na kubaini njia mbadala za kulinda mapato.
Programu hiyo inayojulikana kama Electric Vehicle (EV) Impact Simulator, imetengenezwa kwa msaada wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa Afrika (UNECA), ikiwa na uwezo wa kukadiria mapato yatakayopungua kadri watumiaji wa magari wanavyohama kutoka matumizi ya petroli na dizeli kwenda kwenye magari yanayotumia umeme.

Aidha, programu hiyo ina uwezo wa kujaribu sera na mbinu mbalimbali za mbadala zinazoweza kutumika kurejesha mapato hayo mwaka hadi mwaka kwa kipindi kinachochaguliwa.
Matumizi ya programu hiyo na matokeo yaliyopatikana yaliwasilishwa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka wa ARMFA uliofanyika juzi jijini Nairobi nchini Kenya, ambapo nchi tatu za majaribio ambazo ni Tanzania, Kenya na Msumbiji zilionesha namna programu hiyo inavyofanya kazi.
Katika kikao hicho, uzoefu wa matumizi ya program hiyo uliwasilishwa na Mhandisi Dkt. Joshua Mwankunda kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara Tanzania,amefafanua matumizi ya program hiyo, hususani namna ya kuchakata takwimu muhimu zinzotumika na program katika kukadiria kupungua kwa mapato ya fedha za matengenzo ya barabara pamoja na majaribio ya sera/mbinu mbadala zinazoweza kujazia upungufu huo.
Baada ya uwasilishaji huo, programu hiyo ilikabidhiwa rasmi kwa ARMFA na kupokelewa kwa niaba ya wanachama na Rais wa chama hicho, ambaye pia ni Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Tanzania, Mhandisi Rashid Kalimbaga.
Upokeaji wa programu hiyo unakuja wakati muafaka kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika ambazo zinashuhudia mabadiliko katika sekta ya usafiri kutokana na ongezeko la matumizi ya magari ya umeme.

Mabadiliko hayo yanatoa umuhimu wa kutafuta mifumo mipya na endelevu ya ukusanyaji wa fedha za matengenezo ya barabara kutoka kwa watumiaji wote, ikihusisha aina zote za nishati inayotumika kuendesha vyombo vya usafiri na usafirishaji.
Kupitia teknolojia hiyo, Tanzania pamoja na nchi wanachama wa ARMFA zitakuwa na nyenzo muhimu ya kusaidia kufanya tathmini na kupanga mikakati ya kukabiliana na changamoto za baadaye za upatikanaji wa fedha za matengenezo ya barabara, ili kuhakikisha barabara zinaendelea kutoa huduma endelevu kwa jamii na kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.


More Stories
Makosa ya kibinadamu chanzo MV Mwanza kugonga mwamba
Wananchi waaswa kujitokeza maadhimisho siku ya UKIMWI
Vijana wahimizwa kutumia fursa za ubia miradi ya nishati