November 25, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

120 wafanyiwa uchunguzi wa fistula Chunya

Na Mwandishi wetu, Timesmajira,Online, Mbeya

ZAIDI ya wananchi 120 wamepatiwa elimu ya afya ya uzazi na kufanyiwa uchunguzi wa awali wa ugonjwa wa fistula katika kambi maalum ya siku mbili iliyohitimishwa jana 10/22/2026 wilayani Chunya mkoa wa Mbeya.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha kambi hiyo, Daktari wa Magonjwa ya Kina Mama na Uzazi, Dkt. Antidius Inyasi, amesema mkakati wa kufanyia kambi hiyo katika minada ya Makongolosi na Matundasi umezaa matunda makubwa kwa kuwawezesha kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja na kuvunja ukimya uliopo katika jamii.

“Tumeamua kuwafuata wananchi huku huku kwenye shughuli zao za kiuchumi katika minada ya Makongolosi na Matundasi ili kuondoa vikwazo vya umbali na unyanyapaa. Zaidi ya wananchi 120 wamepata elimu na kufanyiwa uchunguzi, na wale waliobainika kuwa na tatizo tumewapa utaratibu wa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Nyanda za Juu Kusini ambako watapata matibabu kamili,” alisema Dkt. Antidius.

Ameeleza kuwa tatizo kubwa lililoonekana ni pamoja na umbali wa kufwata matibabu, hali ya kipato na gharama za matibabu pia Imani potofu iliyojengeka katika jamii kuhusiana na ugonjwa wa fistula ya uzazi na kuchanika msamba.

Kwa upande wake, Odeta Kapange mmoja wa wananchi waliojitokeza kupata huduma, amemshukuru Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Nyanda za JuuKusini na kupongeza hatua ya wataalamu wa afya kuwafuata vijijini, akieleza kuwa imewapa uelewa mpana na matumaini mapya .

“Wengi wetu tulikuwa hatujui kama huduma hizi zinapatikana na tulikuwa tunaogopa kwenda hospitali kubwa. Kuwakuta madaktari hapa mnadani kumeturahisishia sana; tumepata elimu nzuri, tumefanyiwa uchunguzi bure na waliokutwa na tatizo wamepewa mwongozo wa kwenda kutibiwa Mbeya,” alisema Odeta.

Kambi hiyo iliyoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Afya na shirika la Fistula Foundation, tarehe 23 na 24 novemba 2026 ilifanyika katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kwenye magulio (minada) ya Makongolosi na Matundasi, ikiwa na lengo la kusogeza huduma karibu na jamii na kuibua wagonjwa waliokuwa wakiteseka majumbani.