November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Lugeye waahidiwa ujenzi wa shule

Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Magu kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Boniventura Kiswaga ameahidi kujenga shule katika Kijiji cha Lugeye Wilayani humo ili kuwapunguzia watoto umbali mrefu wa kwenda shule.

Amesema,kinachotakiwa ni wananchi wa kijiji hicho kumtengea eneo litakalotumika kujenga shule ya msingi kwa ajili ya watoto ahadi ambayo ataitekeleza baada ya kuchaguliwa na kuapishwa kuwa mbunge wao.

Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni wakati akiomba kura kwa wananchi wa Kijiji cha Lugeye Kata ya Kitongosima, Kiswaga amesema, bado ana deni kubwa kwa wananchi hao tangu akiwa diwani na kabla ya kugombea Ubunge mwaka 2015 na kuchaguliwa hivyo ili kuwalipa deni hilo, watafute eneo ambalo litakuwa katikati ya vijiji vyote vya Kata ya Kitongosima itakakojengwa shule hiyo ili watoto kutoka vijiji vingine wafike shuleni kwa urahisi.

Amesema, ipo haja ya kujenga shule nyingine ya sekondari ili kuendelea kuboresha elimu na watoto wasome kwa uhakika bila mrundikano darasani.

Pia Kiswaga amesema kuwa, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita amefanikiwa kuwaletea maendeleo wananchi wa Jimbo hilo kwani Wilaya ya Magu ya sasa haifanani na ya zamani ambapo katika sekta ya umeme vijiji vingi vimeunganishwa na nishati hiyo ambapo vijiji vilivyobaki vitapata, huduma hiyo.

Kwenye sekta za elimu na afya maboma yamejengwa , barabara na miradi ya maji huku vikundi vya wajasiriamali vikiwezeshwa kiuchumi kwa kupata mikopo isiyo na riba kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Magu.

“Ndugu zangu watu wa Kitongosima sitaki niseme mengi kwani mmeyaona na kuyashuhudia kwa macho,nikitaja elimu ,maji na afya na umeme nimefanya hivyo nipeni tena mitano nikawatumikie ili maji yafike hapa Lugeye,”.

“Kazi yangu ni kutenda, nilitafuta fedha na Dkt.Magufuli alinipa za kuleta maji hapa, tumeshafunga mashine tatu na jana yameanza kutoka lakini yangeshaanza kutoka tangu wiki nzima tatizo ni sisi wenyewe tunakata mabomba na kusema ni feki, kwa nini lisipasuke bomba lote na unaliona kabisa limekatwa na viungio vimetolewa,nawaombeni sana hamnikomoi mimi bali wananchi wa Kitongosima,” amesema Kiswaga.

Am\esema, bado anahitaji kuwatumikia wananchi wa Jimbo la Magu hivyo wamchague yeye kwa nafasi ya Ubunge,Urais wampe Dkt.Magufuli na Madiwani wanaotokana na CCM ili waendelee kuleta maendeleo.