November 24, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Uchaguzi wa TUCTA wasitishwa na Mahakama Kuu

Na.Mwandishi Wetu,TimesMajira

SAKATA la Uchaguzi la Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA ), lachukua sura mpya baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi kusitisha vikao vyote na uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo uliokuwa umepangwa kufanyika Novemba 25 hadi 27, 2026, jijini Dodoma.

Akisoma uamuzi huo leo mbele ya Waandishi wa habari,Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Saidi Wamba, amesema uamuzi huo umetolewa leo(jana) na mahakama hiyo chini ya Jaji Modesta Opiyo kufuatia hatua iliyochukuliwa na mmoja wa mwanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Ulinzi Binafsi(TUPSE), kufungua shauri mahakamani kwa lengo la kuomba zuio la vikao na uchaguzi mkuu hadi pale mgogoro huo utakapopatiwa ufumbuzi.

Wamba amesema mahakama imeelekeza hali ya uongozi na utendaji wa shirikisho hilo ibaki kama ilivyo sasa, huku pande zote zikisubiri kusikilizwa kwa shauri hilo ambalo litatajwa Novemba 30,2026.

Amesema katika maamuzi , mahakama imezuia TUCTA, mawakala wake, watumishi, wanachama na watu wengine wanaotenda kwa niaba yake kuitisha, kuendesha au kuendelea na mkutano wowote mkuu pamoja na uchaguzi uliopangwa kufanyika Novemba 25, 26 na 27, 2026, Dodoma au eneo jingine lolote.

Amesema shauri hilo litatajwa tena Novemba 30, 2026, kwa ajili ya kusikilizwa kwa pande zote mbili, huku upande wa TUCTA ukipewa jukumu la kuhakikisha uamuzi huo unawafikia wahusika wote.

Kwa upande wake aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa TUCTA ambae ndiye anayeratibu Mkutano huo Mkuu na Uchaguzi,Rehema Ludanga alipotafutwa na waandishi wa habari kama amepata uamuzi huo wa mahakama amesema kwasasa hayupo tayari kuzungumza na mwandishi yeyote.