
Na Mwandishi Wetu,Kenya
Rais wa Umoja wa Mifuko ya Barabara Afrika (ARMFA) na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara Tanzania, Mhandisi Rashid Kalimbaga amesema kuimarisha mifumo endelevu ya ufadhili wa matengenezo ya barabara ni hatua muhimu katika kulinda miundombinu, kukuza biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi barani Afrika.
Akizungumza Novemba 24,2026 wakati wa ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 23 wa ARMFA unaofanyika jijini Nairobi nchini Kenya Mha.Kalimbaga alitaja vipaumbele vitano vya utekelezaji wa majukumu yake ya uongozi wa miaka miwili,ambapo alisisitiza umuhimu wa kuwa na mifumo ya uhakika, uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za matengenezo ya barabara.

Vipaumbele hivyo ni kuhakikisha upatikanaji wa fedha za uhakika kwa ajili ya matengenezo ya barabara, kuimarisha uhuru wa kiutendaji wa Mifuko ya Barabara, kujenga uwezo wa kitaasisi, kuimarisha ushirikiano na ubunifu katika maeneo mbalimbali ya Afrika pamoja na kuongeza ushawishi na mwonekano wa ARMFA katika ngazi ya kikanda na kimataifa.
Amesema mifumo ya ufadhili inapaswa kuwa imara na inayoweza kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi pamoja na mabadiliko ya mapato yatokanayo na watumiaji wa barabara.
Pia amesema,ni muhimu kutafuta vyanzo mbadala vya fedha kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, ufadhili wa tabianchi na mikataba inayozingatia matokeo.
Akizungumzia umuhimu wa uhuru wa Mifuko ya Barabara,Mha.Kalimbaga amesema,mifuko hiyo inapaswa kuwa na uhuru wa usimamizi, rasilimali zinazotengwa kwa matumizi yaliyokusudiwa na mifumo imara ya uwajibikaji ili kujenga imani kwa watumiaji wa barabara na wadau wa maendeleo.
Aidha,ameipongeza Serikali ya Kenya kwa kukubali kuwa mwenyeji wa Makao Makuu ya ARMFA na kueleza kuwa Mkataba wa Nchi Mwenyeji (Host Country Agreement), unaotarajiwa kusainiwa Novemba 26, 2026, utaiwezesha taasisi hiyo kupata utambuzi wa kisheria, uthabiti na uaminifu unaohitajika katika kutekeleza majukumu yake kama taasisi ya bara la Afrika.
Hata hivyo amesema,ARMFA imepiga hatua katika kuanzisha Sekretarieti ya Utendaji, kufanya utafiti wa RRAM kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kuanzisha mafunzo ya awali ya Chuo cha ARMFA, kuunda Kamati ya Kisayansi na kusaini Itifaki ya Ushirikiano na Tume ya Umoja wa Mataifa ya Kiuchumi kwa Afrika (UNECA) huku akionya kuwa bado kuna changamoto katika hali ya miundombinu ya barabara barani Afrika, licha ya umuhimu wake katika kukuza biashara na kuunganisha nchi za bara hilo.
Amebainisha kuwa zaidi ya asilimia 80 ya bidhaa zinazosafirishwa barani Afrika hutumia barabara, hivyo ubora na uimara wa miundombinu hiyo ni muhimu katika kuimarisha biashara ya ndani ya Afrika, hususani kupitia Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA), lenye soko la watu takribani bilioni 1.3.
Akitoa mfano wa mafanikio ya Tanzania Mha.Kalimbaga amesema,mapato ya Mfuko wa Barabara nchini yaliongezeka kwa asilimia 45 katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/20 hadi 2024/25, yakichangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za bandari na usafirishaji wa mizigo ya nchi jirani kupitia Tanzania.
Amesisitiza kuwa ujenzi wa barabara ni mwanzo tu wa uwekezaji katika miundombinu, huku matengenezo yakiwa ndiyo yanayohakikisha barabara zinaendelea kutoa huduma kwa uchumi na wananchi kwa muda mrefu.
Aisha amesisitiza umuhimu wa kufikiwa kwa maamuzi mahususi, yakiwemo kupitishwa kwa dira mpya ya ARMFA na mpango kazi wenye gharama za utekelezaji, kuandaliwa kwa Mpango wa Kuboresha Utawala kwa kila Mfuko wa Barabara na kuendelezwa kwa pendekezo la kuanzisha Mfuko wa Dhamana wa Bara la Afrika kwa ajili ya Matengenezo ya Barabara (FFC-ER).
Mha.Kalimbaga ametoa wito kwa Serikali, washirika wa maendeleo na wadau wa sekta ya barabara kuendelea kushirikiana katika kuimarisha mifumo endelevu ya ufadhili wa matengenezo ya barabara, akieleza kuwa kutunza barabara ni kulinda uwekezaji wa nchi, kuokoa maisha na kuunganisha masoko na wananchi.
Mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo “Mifuko ya Kizazi Kipya ya Matengenezo ya Barabara: Ufadhili wa Kiwango cha Bara, Muunganiko wa Kikanda na Ustahimilivu kwa Afrika Iliyounganishwa” unawakutanisha wawakilishi wa nchi 35 pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya barabara na maendeleo.


More Stories
Dkt.Gwajima azindua chuo cha wasichana
Tantrade kuunganisha Wanawake,Vijana na fursa za Soko la Afrika
Mwigulu ataka tume za uchaguzi SADC kudhibiti upotoshaji mitandaoni