November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wananchi Nkanda, Chanjale wataka Zahanati, walimu

Na David John, TimesMajita Online, Lumbila

WANANCHI wa vijiji vya Nkanda na Chanjale Kata ya Lumbila wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe wamemuomba Mbunge mteule ambaye amepita bila kupingwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu Joseph Kamonga kuwasaidia kutatua changamoto wanazokabiliana nazo hasa ya Zahanati, upungufu wa walimu pamoja na miundombinu ya barabara.

Akizungumza na Mtandao huu kwa niaba ya wananchi wezake wa Kijiji Cha Chanjale, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chanjale, Pascal Haule amesema kuwa, changamoto kubwa ni ukosefu wa Zahanati ambapo wananchi wanalazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya na pia licha ya baadhi ya maeneo kupimwa kwa ajili ya kusogezewa huduma ya maji lakini hadi sasa mabomba hayajawekwa.

“Mwandishi kama mnavyojua vijiji hivi vinapatikana mwambao mwa Ziwa Nyasa na humu kwenye vijiji vyetu kuna mapungufu makubwa ya madarasa kiujumla, mfano hapa shule ya Msingi Chanjale palitakiwa kuwe na madarasa nane lakini yapo sita tu lakini pia walimu wapo watatu wote wanaume tunaomba angalau tungekuwepo sita ,” amesema Mwalimu Haule

Hata hivyo Mtendaji wa Kijiji hicho, Adorati Mwaitulo amesema kuna wakazi 1124 ambao shughuli zao ni za uvuvi na kilimo kidogo na bado wanakabiliwa na changamoto za kukosa umeme na barabara kwani kwa sasa wanayotegemea zaidi usafiri wa majini ili kufika kijiji kingine.

Licha ya kutegemea zaidi uvuvi lakini bado kunakosekana zana zitakazowawezesha kufanya uvuvi bora na kuhusu maji wamesema wake zao wanalazimika kwenye mtoni ambapo ni umbali mrefu hali inayosababisha migogoro ndani ya nyumba zao kutokwisha.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nkanda, Williadi Mwakilambo alimweleza Mbunge huyo mteule kuwa, kuna uhaba mkubwa wa wahudumu kwenye taasisi za serikali lakini pia hawana majengo ya kutosha kwani yapo ambayo hadi sasa wameshindwa kuyamalizia.

Akizungumza kwa niaba ya wazee kutoka ndani ya kata ya Lumbila Kijiji Cha Lumbila, Clement Kaduma amesema, kilio chao ni barabara ya kutoka Ikonda, Iyombo hadi Lumbila kwani kufanikisha kwa barabara hiyo kutatoa urahisi kwao kufanya biashara ,pia urahisi kwenda Hospitali ya Ikonda.

Pia amesisitiza kuwa kwenye elimu afatilie upatikanaji wa walimu shule za msingi Lumbila, Chanjale na Ikanda ambapo shule ya Msingi Chanjale kuna walimu wawili, Lumbila walimu watatu na Ikanda walimu wanne.

Licha ya changamoto hizo wao kama wazee wanamuomba Mbunge huyo kuwahakikishia wanapata kadi za matibabu bure kama serikali ilivyoelekeza huku Mzee Laurent Mwalupale akijitolea mafano kuwa ana miaka 85 lakini hana kadi ya matibabu.

Diwani wa Kata hiyo ya Lumbila, Fortunatus Mwakilambo Akizungumza mbele ya wananchi amesema, yeye kama Diwani mtarajiwa anaahidi kukamilisha Ofisi ya Serikali ya Kijiji cha Ikanda atapigania uwepo wa nyumba za walimu na kuhamasisha wananchi kukaa kwenye vikundi na kupata mikopo kupitia Halmashauri ya Ludewa.

Akijibu maombi hayo, Mbunge huyo mteule mewaeleza wananchi kuwa, jukumu kubwa walilonalo ni kuhakikisha wanamchagua mgombea Urais wa CCM Dkt. John Magufuli na Madiwani wake ili kwa pamoja kwenda kupigania kutatua changamoto walizozibainisha.

“Nawaomba ndugu zangu Oktoba 28 msifanye makosa mimi changamoto zenu nimezichukuwa na tutazifanyia kazi mara tu baada ya uchaguzi mkuu na kwa mapenzi haya mnayoyaonyesha niseme ninadeni kubwa kwenu,” amesema Kamonga.

Kuhusu changamoto za wahudumu wa taasisi za umma hususani walimu amesema, kuna jumla ya upungufu wa walimu 421 hivyo ameshamueleza Makamu wa Rais wakati alipokwenda kwa ajili ya Kampeni hivyo watapata walimu na wahudumu wengine.