Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) limewaomba radhi wateja wake katika Mikoa ya Mbeya na Songwe kutokana na kukosekana kwa huduma ya umeme kufuatia ajali ya kuanguka kwa nguzo ya kusafirisha umeme katika eneo la Inyala, Mkoani Mbeya.
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano na Huduma kwa Wateja ya TANESCO, imeeleza kuwa ajali hiyo imetokana na kuanguka kwa nguzo (tower) ya njia mpya ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 400 ya Mradi wa TAZA, ambayo imeangukia miundombinu ya njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovoti 220 inayosafirisha umeme kutoka Iringa kwenda Mbeya.
Kutokana na ajali hiyo, huduma ya umeme imekatika katika Mikoa ya Mbeya na Songwe, hali iliyosababisha usumbufu kwa wateja wanaotegemea huduma hiyo katika shughuli zao za kila siku.
TANESCO imesema tayari wataalamu wake wamefika katika eneo la tukio na wanaendelea na jitihada za kurekebisha miundombinu iliyoathirika ili kuhakikisha huduma ya umeme inarejea kwa wateja wa mikoa hiyo.

Hata hivyo, Shirika hilo limeeleza kuwa kutokana na ukubwa wa uharibifu uliotokea, huenda zoezi la kurejesha huduma ya umeme likachukua muda mrefu, huku likiahidi kuendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya ukarabati.
Aidha, TANESCO imewaomba wateja wake kuwa na uvumilivu wakati wataalamu wakiendelea kushughulikia changamoto hiyo ili kurejesha huduma ya umeme katika hali ya kawaida

More Stories
TUCTA yaahirisha uchaguzi, Naibu Katibu Mkuu asimamishwa
Umoti:Huhitaji kumpigia mtu simu kupata mafao ya PSSSF
BBM Festival 2026 ya EXIM kulinda madereva