Na mwandishi wetu


SERIKALI imetumia zaidi ya Sh. milioni 600 kujenga miundombinu ya Kituo cha Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima mkoa wa Iringa, ikiwemo madarasa, jengo la utawala, vyoo, chumba cha kulelea watoto wadogo pamoja na bweni lenye uwezo wa kupokea wanafunzi 80.
Uwekezaji huo umefanyika kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP), ulioanza mwaka 2022. Kituo hicho ni kituo mama kinachosimamia vituo vingine vinne vinavyotoa elimu ya sekondari kwa njia mbadala mkoani Iringa, hivyo maboresho hayo yanaimarisha pia uratibu na usimamizi wa huduma za elimu katika vituo hivyo.
Mkufunzi Mkazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Mkoa wa Iringa, Kassim Dallu, amesema kabla ya utekelezaji wa mradi huo kituo kilikabiliwa na changamoto ya miundombinu isiyokidhi mahitaji ya ufundishaji na ujifunzaji, hali iliyokuwa ikiathiri utoaji wa huduma za elimu.
Amesema katika awamu ya kwanza, kituo kilipokea Sh. milioni 397.3 zilizotumika kujenga madarasa manne, jengo la utawala, vyoo vya matundu manne na chumba cha kulelea watoto wadogo, miundombinu ambayo tayari inatumika.
Aidha, amesema katika awamu ya pili kituo kimepokea Sh. milioni 206.7 kwa ajili ya ujenzi wa bweni, ambao unakaribia kukamilika. Bweni hilo litakapokamilika litakuwa na uwezo wa kupokea wanafunzi 80 na kusaidia kupunguza changamoto za malazi kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali ambao walikuwa wakilazimika kupanga makazi mtaani ili kuhudhuria masomo.
Amesema maboresho hayo yameimarisha mazingira ya kujifunzia na kuchangia ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na programu za elimu ya sekondari kwa njia mbadala, ambapo usajili umeongezeka kutoka wanafunzi 188 mwaka 2022 hadi 255 mwaka 2026, huku ukiwa wanafunzi 220 mwaka 2023, 212 mwaka 2024 na 254 mwaka 2025.
Ameongeza kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo umetoa ajira za muda kwa mafundi na vibarua, huku wafanyabiashara wadogo wakinufaika na shughuli za kiuchumi. Aidha, majengo hayo yanatumika kwa shughuli za kielimu na kijamii, ikiwemo mitihani na programu za ujifunzaji kwa njia ya masafa.

More Stories
Maajabu ya aliyekatisha masomo kwa ujauzito
Taasisi huduma ndogo za fedha zatakiwa kuimarisha usimamizi mikopo
Taasisi zatakiwa kuimarisha utayari dhidi ya El Nino