Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
MKURUGENZI Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), James Mbalwe ameikaribisha kampuni mpya ya BetSasa na kuitaka kuzingatia maadili na ustawi wa vijana kwa maendeleo ya jamii.
Mbalwe amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa kampuni ya BetSasa na kampeni ya kuwazawadia wateja wa kampuni hiyo zawadi mbalimbali ikiwemo gari jipya aina ya Jetour.
“Tunawakaribisha BetSasa katika soko la Tanzania, tumeona wameanza vizuri kwa kuja na kampeni hii inayolenga kuwazawadia wateja wao zawadi zenye thamani kubwa ikiwemo gari jipya la kisasa.
“Hata hivyo, tunatoa wito kwao na kampuni nyingine katika sekta hii kuongeza tija ya shughuli zao kwa kuhakikisha wanarejesha kwa jamii kusaidia sekta za afya, elimu, michezo na maeneo mengine muhimu ya maendeleo,” amesema Mbalwe.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa BetSasa, Jimmy Kenneth amesema kampeni hiyo ya mwaka mmoja iitwayo ‘Kusanya Point usepe na Jetour’ inahusisha zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslim.
“Promosheni hii ni mahususi kwa wadau na wateja wa BetSasa hivyo kila wiki zitatoka zawadi mbalimbali na kila baada ya miezi mitatu mshindi mmoja atapata gari jipya aina ya Jetour,” amesema Kenneth.
Kwa mujibu wa Ofisa Mtendaji Mkuu huyo, BetSasa imejipanga kuendesha shughuli zake kwa kuzingatia Sheria, kanuni, masharti, taratibu na muongozo ya mamlaka zinazosimamia michezo ya kubahatisha na kutekeleza wajibu wake kwa jamii.

More Stories
Magereza,VETA kushirikiana kurasimisha ujuzi kwa wafungwa
Ufugaji samaki wachochea Serikali kupanga kuwawezesha viwanda vidogo
Serikali kuchunguza ajali ya Mv.Mwanza