November 17, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wahimizwa kutumia soko la Uturuki kuuza mazao kilimo

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Dar

NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt.Ngwaru Maghembe, amewahimiza wafanyabiashara kutumia fursa ya soko la Uturuki litakalofunguliwa na Serikali kwa ajili ya kuuza mazao mbalimbali ya kilimo yanayozalishwa hapa nchini.

Dkt. Maghembe ametoa wito huo wakati akizungumza na wanahabari kuhusu ushiriki wa Tanzania katika Mkutano wa COP31, uliofanyika Ikulu jijini Dar-es-Salaam.

Amesema,Serikali imepanga kufungua soko la Uturuki kwa mazao mbalimbali ya kilimo yakiwemo chai, kahawa na tumbaku, hatua inayolenga kuongeza fursa za kibiashara kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania.

Amesema kupitia mpango huo, Serikali inalenga kuunganisha kampuni na wafanyabiashara wa Tanzania na wanunuzi pamoja na wawekezaji kutoka Uturuki ili kuwezesha upatikanaji wa masoko mapya ya bidhaa zinazozalishwa nchini.

“Mpango huo unalenga kutangaza bidhaa za Tanzania nchini Uturuki na kuwawezesha wafanyabiashara kukutana na wanunuzi, kujenga mahusiano ya kibiashara na kupanua masoko ya bidhaa zao,” amesema.

Aidha, amewataka wafanyabiashara kutumia fursa hiyo kwa kuhakikisha bidhaa zao zinakuwa na ubora unaokidhi viwango vya kimataifa na kuongeza thamani ya mazao hayo ili yaweze kushindana katika soko la Uturuki.