Na Mwandishi Wetu TimesMajira Online, Mwanza
SERIKALI imekamilisha asilimia 90 ya mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Mwanza Kaskazini, unaogharimu sh. bilioni 18.6,ikiwa ni mkakati wa kuimarisha usafiri na usafirishaji kwa njia ya maji, kukuza biashara na kuongeza ufanisi wa huduma za bandari.
Waziri wa Uchukuzi, Pro.Makame Mbarawa,ametoa kauli hiyo jijini hapa Novemba 16,2026 baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo,ambapo amesema Serikali imeweka kipaumbele katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya kisasa ya bandari ili kutoa huduma bora, salama na endelevu kwa wananchi.

Amesema uboreshaji wa bandari hiyo umeleta mabadiliko katika uwezo wa kuhudumia meli na abiria, ikiwemo kuongeza kina cha maji kutoka mita 3.5 kabla ya mradi hadi mita tano kwa sasa.
Gati lina uwezo wa kuegesha meli sita kwa wakati mmoja, ikiwemo meli ya MV.Mwanza huku jengo jipya la abiria lina uwezo wa kuhudumia watu 700 kwa wakati mmoja, tofauti na jengo la zamani lililokuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 350.
Pia amesema,mradi huo unahusisha ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ikiwemo jengo la abiria, ghala la kuhifadhi shehena ya mizigo lenye uwezo wa tani zaidi ya 50, 000, ujenzi wa kingo za ziwa pamoja na upanuzi wa maeneo ya kuegesha meli na magari.
Prof.Mbarawa amesema, Bandari ya Mwanza Kaskazini ni kitovu cha usafirishaji wa abiria na mizigo katika Ziwa Victoria, uboreshaji wake utaongeza ufanisi wa shughuli za usafirishaji na biashara ndani na nje ya nchi.
Vilevile amesema, Serikali imeendelea kuboresha bandari za Kanda ya Ziwa kwa kutambua mchango wake katika kukuza uchumi, akitaja uwekezaji wa sh. bilioni 18.6 katika Bandari ya Mwanza Kaskazini, sh. bilioni 20.3 katika Bandari ya Kemondo na sh. bilioni 19.5 katika Bandari ya Bukoba.
Hata hivyo amesema,kukamilika kwa uboreshaji wa bandari hizo kutatoa fursa kwa wafanyabiashara wa mikoa ya Kanda ya Ziwa na nchi jirani kutumia usafiri wa majini kusafirisha bidhaa zao badala ya kutegemea malori pekee, hivyo kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza usalama wa abiria na mizigo.
Katika hatua nyingine, Prof.Mbarawa amesema Serikali imejenga meli ya kisasa ya MV.Mwanza yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo na magari 10,ambayo inatarajiwa kutoa huduma ndani ya Ziwa Victoria na kuunganisha Tanzania na nchi jirani za Kenya na Uganda ili kuongeza fursa za biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.
“MV.Mwanza tunataka iende nchi jirani za Kenya na Uganda, ili kukuza biashara na mataifa hayo na kuchangia uchumi wa nchi. TPA asilimia 90 tumemaliza, sasa simikeni maboya na minara ya kuongozea meli ziwe salama,” amesema.
Kadhalika amesema,asilimia 10 ya kazi zilizobaki kukamilisha mradi huo hazitakuwa kikwazo kwa meli hiyo kuanza kutoa huduma, baada ya kukamilika kwa gati, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na Kampuni ya Huduma za Meli Tanzania (TASHICO) zitakutana kupanga ratiba za safari kwa kuzingatia mahitaji ya kibiashara na wananchi.

Aidha amesema,uwekezaji katika miundombinu ya bandari ni utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga uchumi imara, jumuishi na wenye ushindani wa kimataifa, hivyo sekta binafsi itumie fursa zilizopo kuwekeza katika sekta ya usafirishaji, ushiriki wake utasaidia kuongeza ufanisi, kupanua huduma na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA),Plasduce Mbossa amesema,
maboresho hayo yanayofanywa na Serikali yataifanya bandari hiyo kutoa huduma zenye ushindani, kukuza biashara na kuongeza ufanisi katika kuhudumia abiria na shehena ya mizigo kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.

More Stories
Serikali yaendelea kuimarisha uratibu maandalizi AFCON 2027
Tanzania kuwakutanisha nchi za Afrika kujifunza Afya ya Mama na Mtoto
Wahimizwa kutumia soko la Uturuki kuuza mazao kilimo