November 16, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas, Mixx zaunga mkono Lake Victoria Marathon

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI za Yas na Mixx zimeunga mkono juhudi za kuboresha huduma kwa watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) kupitia udhamini wao wa msimu wa sita wa Lake Victoria Marathon.

Mbio hizo ziliwakutanisha wakimbiaji na wadhamini kwa lengo la kukusanya michango kwa ajili ya watoto hao. Pia zilitumika kuhamasisha mazoezi ya mwili na utunzaji wa Ziwa Victoria.

Akizungumza katika hafla ya kufunga mbio hizo jijini Mwanza leo,  Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiri Mkalipa amesema tukio hilo limeonyesha namna michezo inavyoweza kuziunganisha jamii katika kutatua mahitaji ya wananchi.

“Mbio hizi zimetupa nafasi ya kufanya mazoezi na kuhamasishana kuhusu afya, huku tukiwakumbuka watoto njiti wanaohitaji huduma maalumu. Nawapongeza waandaaji, wadhamini Yas na Mixx na wadau wengine kwa kuunga mkono jitihada hizi,” amesema Mkalipa.

Amewataka wananchi kufanya mazoezi mara kwa mara na kuendelea kulinda Ziwa Victoria hata baada ya mbio hizo, akisema ziwa hilo ni muhimu kwa jamii za kanda nzima ya ziwa.

“Wakazi wengi wanategemea Ziwa Victoria kwa chakula, ajira na biashara. Kila mmoja ana wajibu wa kulitunza ili liendelee kutunufaisha sisi na vizazi vijavyo,” amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Yas, Kanda ya Ziwa Magharibi, Daniel Mainoya amesema Yas na Mixx zimeamua kudhamini mbio hizo kwa sababu zinawapa watanzania fursa ya kuchangia ustawi wa jamii kupitia michezo.

“Nawashukuru waandaaji kwa kutumia mbio hizi kukusanya michango kwa ajili ya watoto njiti. Iwe umekimbia kwa ajili ya ushindani, kuboresha afya au kufurahi na wapendwa wako, ushiriki wako una umuhimu mkubwa,” amesema Mainoya.

Amesema, mbio hizo pia zinajenga ushirikiano na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kulinda maliasili zinazotegemewa kwa maisha ya wakazi wa Kanda ya Ziwa.

Kwa upande wake, Mratibu wa Lake Victoria Marathon, Hilda Viggo amesema “Tunawashukuru Yas na Mixx, wadhamini wengine na washiriki wote kwa kuwa sehemu ya msimu huu wa sita.

“Lengo letu limekuwa ni kutumia mbio hizi ili kuhamasisha mazoezi, lakini pia kuunga mkono huduma za kijamii na kwa mwaka huu sehemu ya mapato yataenda kwa watoto njiti na kutunza mazingira ya Ziwa Victoria,” amesema Viggo.