Na Fresha Kinasa,TimesMajira Online,Mara
MGODI wa Dhahabu wa Barrick North Mara uliopo Nyamongo, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, umezindua Wiki ya Mahusiano (Mahusiano Week) inayolenga kuendelea kuimarisha mahusiano bora baina ya mgodi huo na wananchi wa vijiji vinavyouzunguka.
Wiki hiyo imezinduliwa Novemba 14, 2026 katika uwanja wa Ingwe Sekondari uliopo Nyamongo ambapo makundi mbalimbali ya viongozi wa Serikali, mgodi pamoja na wananchi wameshiriki mbio za km 3 tatu.

Kauli mbiu ya wiki hiyo ya mahusiano inasema ‘Mahusiano Bora kwa Uwekezaji Endelevu’,ambapo michezo mbalimbali itafanyika katika vijiji vyote 11 vinavyozunguka mgodi huo na washindi watapewa zawadi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele amesema, mahusiano bora ni msingi wa maendeleo kati ya wananchi na mgodi huo huku michezo itakayofanyika itaimarisha zaidi umoja na afya.
“Mahusiano bora ni msingi wa maendeleo, michezo hii itaimarisha umoja na afya za vijana wetu.Niupongeze mgodi kwa jitihada mbalimbali ambazo umekuwa ukizifanya kuimarisha mahusiano haya, ambayo yanafaida kwa pande zote mbili,”amesema Gowele.
Mkuu huyo wa Wilaya pia amesema Serikali inatambua na kuthamini kikamilifu maendeleo yanayofanywa na mgodi huo kupitia fedha za CSR, ambazo zimeendelea kuimarisha maendeleo wilayani humo.
Pia, amewataka vijana wa vijiji vinavyozunguka mgodi huo, kuacha kuvamiana kufanya shughuli za uchimbaji katika eneo la mgodi wa Barrick North Mara kwani ni kosa kisheria.
Hata hivyo amewaagiza viongozi wa Kata na Vijiji kukemea uvamizi katika eneo la mgodi , kwani unaweza kuathiri uzalishaji na wananchi kukosa fedha ambazo zimekuwa zikisaidia miradi ya maendeleo katika maeneo yao kupiti uwajibikaji kwa jamii CSR.
Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi amesema, lengo la kuwa na” Mahusiano Week” ni kujenga mahusiano bora na jamii inayozunguka mgodi huo, pamoja na kuhamasisha suala la kujenga afya bora kupitia michezo mbalimbali itakayofanyika katika vijiji hivyo.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Steven Doyle amesema, kwa sasa ongezeko la vijana kuvamia eneo la mgodi huo limeongezeka licha ya juhudi za Serikali na uongozi wa mgodi kupambana na kitendo hicho,hivyo amewataka wazazi na walezi kuwazuia watoto wao wasifanye hivyo kwani kunaweza kuathiri uzalishaji wa mgodi huo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC), Rashid Bugomba amesema,”Mahusiano Week” itawaimarisha vijana kushiriki michezo na kuibua vipaji kwa wanaopenda michezo, huku akipongeza hatua kubwa za kimaendeleo ambazo zimeendelea kufanywa na mgodi huo, zikigusa nyanja mbalimbali ikiwemo elimu, barabara, afya, maji na michezo.
Bhoke Shadrack, mkazi wa Nyamongo, ameushukuru mgodi huo kwa namna ambavyo umewezesha maendeleo katika nyanja mbalimbali, jambo ambalo amesema linatokana na mahusiano bora ambayo mgodi huo umeendelea kuyaimarisha kwa njia mbalimbali.


More Stories
Rhino Rangers yapewa nguvu ya kupanda Ligi Kuu
AFDB kuipatia Tanzania Dola Milioni 26 za Mabadiliko ya Tabianchi
Tanesco yatumia michezo kuendeleza Kampeni ya Pika kwa Umeme