Na Mwandishi Wetu,TimesMajira
MKUU wa Wilaya ya Kilosa, Shaka Hamdu Shaka, amemshukuru na kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuimarisha bajeti ya ulinzi, kuwekeza katika mafunzo na kudumisha amani nchini.
“Leo Tanzania ni kisiwa cha amani. Bila usalama hakuna maendeleo. Kiwanda hakiwezi kuzunguka, shamba haliwezi kulimwa, mwanafunzi hawezi kusoma kama nchi haina amani,”amesema Shaka
Shaka ameyasema hayo leo katika Viwanja vya Mpira Kilosa Town, wakati akifunga rasmi mafunzo ya Jeshi la Akiba Kundi la 21/26 kwa mwaka 2026 yaliyodumu kwa miezi minne.

Amewapongeza wahitimu kwa nidhamu na uzalendo, na kuwataka kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 27 katika kuhakikisha wanailinda nchi kwa wivu mkubwa, kukataa kutumiwa kwenye mitandao kusambaza uongo na uchochezi, na kuwa mfano wa nidhamu mtaani.
“Mliingia raia, leo mnatoka askari. Nendeni mkaitumikie nchi kwa uaminifu – Mungu, Nchi, na Rais.” – Shaka
Kuhusu mchango wa Jeshi la Akiba katika maendeleo ya nchi, Shaka amewataka wahitimu hao wakirudi kata na vijiji vyao, wasaidie Halmashauri kulinda mapato ya umma, kusimamia minada na masoko, na kushirikiana na Polisi Kata pamoja na vyombo vingine kulinda rasilimali za nchi.

“Kijiji kimoja salama, kata salama, wilaya salama, mkoa salama – na hatimaye Tanzania salama.” – Shaka
Hata hivyo, DC Shaka amewaonya wahitimu hao dhidi ya maadui wawili wasioonekana – dawa za kulevya na UKIMWI, akisema bado ni janga linaloteketeza nguvu kazi ya Taifa letu.
“Askari hodari ni yule anayejua kulinda mwili wake kama anavyolinda bunduki yake.” – Shaka



More Stories
Lissu atiwa hatiani kwa uchochezi
Wadau waaswa kuwafikia wananchi wanaoishi Pembezoni
Asas apokelewa kwa kishindo Songwe