Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), kwa kushirikiana na Heart Team Africa Foundation (HTAF), inalenga kukusanya shilingi bilioni 25 kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto 1,000 wenye magonjwa ya moyo nchini, kupitia hafla ya JKCI–HTAF Prestige Gala Dinner 2026.
Akizungumza kuhusu hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dkt. Peter Kisenge, amesema Tanzania ina wataalamu na uwezo wa kutoa huduma za upasuaji wa moyo kwa watoto, hivyo ushirikiano wa Serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali ni muhimu katika kuhakikisha watoto wenye uhitaji wanapata matibabu kwa wakati.
Hafla hiyo inatarajiwa kufanyika Desemba 4, 2026, katika Hoteli ya Malaika Beach Resort jijini Mwanza, chini ya kaulimbiu “Okoa Moyo wa Mtoto, Okoa Taifa,” huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Dkt. Kisenge amesema fedha zitakazokusanywa zitalenga kugharamia matibabu ya watoto 1,000 wenye magonjwa ya moyo katika kipindi cha miaka minne hadi mitano, pamoja na kusaidia ujenzi wa Nyumba ya Matumaini itakayowasaidia watoto wanaopatiwa matibabu na familia zao.
Aidha, amesema changamoto inayowakabili baadhi ya watoto wenye magonjwa ya moyo nchini si ukosefu wa wataalamu pekee, bali pia uwezo wa familia zao kumudu gharama za matibabu, hali inayofanya ushirikiano wa wadau mbalimbali kuwa muhimu katika kuwasaidia watoto hao.
Pia amesema kuwa Serikali hugharamia asilimia 70 ya gharama za matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo, huku mzazi au mlezi akiwajibika kulipa asilimia 30 inayobaki, lakini baadhi ya familia hushindwa kumudu sehemu hiyo kutokana na hali ngumu za kiuchumi, jambo linaloweza kuchelewesha upatikanaji wa huduma za matibabu.
Makadirio yaliyotolewa yanaonesha kuwa watoto 16,000 hadi 24,000 wanaweza kuzaliwa na matatizo ya moyo nchini kila mwaka, huku takribani watoto 4,000 kati yao wakikadiriwa kuwa na magonjwa makali ya moyo yanayohitaji upasuaji ndani ya mwaka mmoja. Kupitia ushirikiano huo, JKCI na HTAF zinalenga kuongeza fursa za watoto kupata matibabu kwa wakati na kupunguza changamoto zinazokabili familia zao.

More Stories
OTR yataka mikopo ya SELF kuleta matokeo
TANESCO yafunga transfoma ya mva 150 kuimarisha umeme
Mfuko wa SELF watoa mikopo ya Bil.138