October 28, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

TTCL yatangaza kutoa ofa ya fiber mlangoni kwako

Na Penina Malundo,TimesMajira

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limezindua kampeni ya msimu wa bure kwa wateja wa huduma ya Fiber Mlangoni Kwako, inayolenga kuwawezesha Watanzania kupata huduma za intaneti na mawasiliano kwa gharama nafuu katika kipindi cha mwisho wa mwaka.

Kupitia kampeni hiyo, wateja wapya na waliopo watakaolipia kifurushi cha Triple Hub cha Sh 70,000 au zaidi watanufaika na vifaa na huduma mbalimbali bila gharama za ziada, ikiwemo simu ya mezani, ruta (router), laini tatu za simu na huduma ya burudani ya T-Burudani.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kuhusu kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL, Vedastus Mwita, amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha Watanzania kuendelea kuwasiliana na kutumia intaneti kwa urahisi, hususan katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka.

Amesema huduma ya Fiber Mlangoni Kwako imekuwa sokoni kwa zaidi ya miaka miwili, ikihudumia makundi mbalimbali ya wateja, yakiwemo familia, wafanyabiashara wadogo na maeneo yenye shughuli za kijamii.

Mwita amesema TTCL imeendelea kuboresha huduma hizo kwa kutumia teknolojia mbalimbali kulingana na mabadiliko ya teknolojia duniani, ambapo kwa sasa inatumia teknolojia ya kisasa ya XGPON.

Ameeleza kuwa kampeni hiyo imekuja katika kipindi ambacho familia nyingi hukutana nyumbani kutokana na likizo za mwisho wa mwaka na kufungwa kwa shule, hivyo kuongeza umuhimu wa huduma bora za intaneti katika mawasiliano na burudani.

“Tunafahamu kuwa wateja wetu wanahitaji huduma zinazowawezesha kuendelea kuwasiliana wanapokuwa nyumbani na hata wanapokuwa nje ya nyumba zao. Ndiyo maana tumekuja na kifurushi cha Triple Hub kinachowawezesha kufurahia huduma hizo,” amesema.

Kwa mujibu wa Mwita, mteja atakayejiunga na kifurushi cha Triple Hub cha Sh 70,000 au zaidi atapatiwa simu ya mezani na ruta bila malipo, huku simu hiyo ikiunganishwa moja kwa moja kwenye ruta ili kumwezesha kupiga simu kwa mujibu wa masharti ya kifurushi chake.

Aidha, mteja huyo atapewa laini tatu za simu zitakazomwezesha yeye na wanafamilia kutumia huduma za intaneti kupitia simu za mkononi wakiwa maeneo mbalimbali nchini Tanzania, kwa mujibu wa masharti ya huduma hiyo.

Amesema wateja hao pia wataunganishwa na huduma ya T-Burudani, inayowawezesha kutazama filamu, tamthilia na maudhui mengine ya burudani.

Mwita amesema wateja wapya wanachotakiwa kufanya ni kujaza fomu za kuomba huduma ya Fiber Mlangoni Kwako na kuchagua kifurushi cha Triple Hub cha Sh 70,000 au zaidi. Baada ya kukamilisha taratibu hizo, timu ya TTCL itafika kuwaunganishia huduma pamoja na kuwapatia vifaa vilivyoainishwa kwenye kampeni hiyo.

Kwa upande wa wateja waliopo,amesema wale wanaotumia kifurushi cha Sh 55,000 wanaweza kunufaika na ofa hiyo kwa kuboresha vifurushi vyao kwenda Triple Hub ya Sh 70,000 au zaidi.

Ameongeza kuwa wateja hao wanapaswa kufika katika ofisi au maduka ya TTCL yaliyo karibu nao wakiwa na namba zao za huduma (service number) ili kuhakikiwa na kupatiwa vifaa na huduma zinazotolewa kupitia kampeni hiyo.

Amesema kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za shirika hilo kupanua matumizi ya intaneti na kuwawezesha wateja kutumia huduma zao za nyumbani hata wanapokuwa safarini au katika maeneo mengine.

Mwita amebainisha kuwa huduma hiyo itapatikana katika maeneo ambayo TTCL imeweka miundombinu ya Fiber Mlangoni Kwako, yakiwemo Dar es Salaam, Arusha, Dodoma, Mwanza, Mbeya, Iringa na Unguja, Zanzibar.

Amewahimiza Watanzania wanaoishi katika maeneo yenye huduma hiyo kutembelea ofisi na maduka ya TTCL ili kupata maelezo zaidi na kujiunga na kifurushi kinachowawezesha kunufaika na ofa hiyo.

Amesema kupitia kampeni hiyo, wateja wataweza kutumia intaneti ya nyumbani na kuendelea kuwasiliana na familia zao wakiwa katika maeneo mbalimbali, bila kulazimika kutegemea vifurushi tofauti vya intaneti kila wanapokuwa nje ya nyumba zao, kwa kuzingatia masharti ya huduma husika.