December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mpinzani wa Kiduku kutua Oktoba 24

Na Yusuph Digossi, TimesMajira Online

WAKATI bondia wa kimataifa wa Tanzania ambaye ameshawahi kushinda ubingwa wa IBF, UBO na Ubingwa wa Taifa, Twaha Kassim ‘Kiduku’ akiwa katika maandalizi ya mwisho kabisa kuelekea pambano lake la kuwania ubingwa wa Dunia wa WBC, mpinzani wake Sirimongkhon Lamthuam kutoka nchini Thailand anatarajiwa kutua hapa nchini Oktoba 24.

Sirimongkhon atatua hapa nchini siku tano kabla ya pambano hilo la raundi 12 la uzani wa Super Middle Welter litakalofanyika Oktoba 30 katika ukumbi wa PTA.

Bondia huyo mwenye rekodi ya kibabe atatua hapa nchini akiambatana na wasaidizi wake wawili ambao ni kocha na meneja wake kuelekea pambano hilo litakaloamuliwa na waamuzi kutoka nje ya nchi na Mtanzania mmoja.

Pambano hilo litasimamiwa na refa Filermon Mweya atakayetokea nchini Namibia, jaji namba moja atakuwa John Chagu wa Tanzania, jaji namba mbili ni Lynette Onam kutoka Kenya, jaji namba tatu ni Iren Semaya toka Uganda na msimamizi wa pambano hilo atokea nje ya nchi.

Licha ya bondia huyo mwenye miaka 43 kumzidi Kiduku miaka 15 lakini rekodi zinambeba zaidi Mthailand huyo ambaye anatamba kwa rekodi nzuri aliyoiweka kwani katika mapambano 101 aliyocheza ameshinda mapambano 97, 62 kwa KO na kupoteza mapambano manne wakati Kiduku ambaye ameshacheza mapambano 22 ameshinda 15, nane kwa KO amepoteza mapambano sita na kutoa sare katika pambano moja.

Katika pamambano mawili ya kimataifa waliyopigana kabla ya pambano hilo, Sirimongkhon ameshinda kwa KO katika pambano lililoganyika Septemba Mosi, 2018 na kwa TKO Desemba Mosi, 2019 huku Kiduku akipoteza kwa TKO, Septemba 16, 2019 lakini pia akishinda kwa TOK katika pambano la Novemba 29, 2019.

Akizungumzia maandalizi yake, Kiduku amesema kuwa, hadi sasa ameshamaliza asilimia kubwa ya maandalizi yake chini ya makocha wake Power Ilanda na Simon Ponera jambo linalompa uhakika ya kuweka rekodi mpya katika pambano hilo na jambo zuri wote wanatumia mtindi mmoja wa ‘Orthodox’.

Licha ya rekodi zake kuzidiwa zaidi ya nne na mpinzani wake lakini amesema hatojali kwani anachokitaka ni kuweka heshima mpya katika pambano hilo ambalo linamfanya kuwa bondia wa kwanza kutoka nchini kuwania ubingwa huo.

Kiduku amesema, kwakuwa kwake kucheza pambano hilo la kuwania mkanda wa WCB unaotambulika Dunia nzima ni heshima kubwa, makocha wake waliamua kumzidishia dozi ya mazoezi ambayo yalijikita zaidi kufanyia kazi mapungufu ya mpinzani wake waliyoyaona kujirudia katika mapam bano yake mbalimbali.

“Ubora na rekodi za mpinzani wangu ziliwafanya makocha wangu kunipa mazoezi magumu ambayo pia yanajikita katika makosa ya mpinzani wangu ili kunifahisishia kumaliza pambano mapema, kwa sasa namuomba Mungu anijaalie afya iliyo njema ili kufanya mambo mazuri katika siku ya pambano langu na kuendelea kuipeperusha vema bendera ya nchi yangu ,” amesema Kiduku.