Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online,Tanga
WAKATI mapambano dhidi ya dawa za kulevya yakiendelea hapa nchini, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo inakabiliwa na changamoto ya kuwafuatilia waraibu 436 walioacha kufika kliniki ya Methadone, kati ya watu 1,390 waliosajiliwa kupata huduma hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 2020.
Hali hiyo inaibua umuhimu wa kuimarisha ufuatiliaji wa wagonjwa na kuongeza ushiriki wa jamii katika kuwasaidia watu wenye uraibu kurejea katika maisha ya kawaida.

Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Tanga, Halid Rashed jana katika mafunzo ya kinga dhidi ya dawa za kulevya yaliyowakutanisha Maofisa Maendeleo ya Jamii,Maofisa Ustawi wa Jamii, madaktari, walimu na makundi ya vijana alisema,pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali, tatizo hilo bado linaendelea kuathiri jamii na linahitaji ushiriki wa wadau wote.
Amesema,ukaribu wa Mkoa wa Tanga na nchi jirani pamoja na mwambao wa Bahari ya Hindi ni miongoni mwa mazingira yanayoweza kutumiwa na wahalifu kuingiza dawa za kulevya, hivyo alisisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu kwa umma na ushirikiano katika kubaini wanaojihusisha na biashara hiyo.
“Ni kweli tuna waraibu wengi ambao wameanza kutumia dawa za kupona, lakini bado kuna watu wengine ambao hawajatambuliwa na wako mtaani. Jambo hili linatusikitisha sana kama halmashauri,”amesema Rashid.
Ameeleza kuwa halmashauri inaendelea kuweka mikakati ya kutoa elimu kuanzia ngazi za mitaa, huku akiwataka viongozi wa Serikali za Mitaa na Kata kushirikiana na wananchi kubaini wanaojihusisha na uingizaji na uuzaji wa dawa hizo.
“Ninachotaka kuwaambia waingizaji wote wa dawa za kulevya kutoka nje na ndani ya nchi ni kwamba waache, kwa kuwa wanawaathiri vijana wetu ambao ndio nguvu kazi ya Taifa,”amesema.
Sanjari na hayo amewataka wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kuwafichua wanaojihusisha na uingizaji na biashara ya dawa za kulevya, akiwalaumu kwa kutanguliza maslahi binafsi huku wakihatarisha maisha ya vijana ambao ni nguvu kazi ya taifa.
Hata hivyo takwimu za huduma ya Methadone katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo zinaonesha kuwa kati ya waraibu 1,390 waliosajiliwa tangu mwaka 2020, watu 102 wamefariki, 490 wanaendelea kupata huduma na 203 wamekamilisha matibabu huku 436 wameacha kufika kliniki ambapo juhudi za kuwafuatilia zikiendelea.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa kuwafikia wagonjwa hao, Mfamasia katika Kitengo cha Methadone Bombo, Fatuma Ismail amesema,kituo kinaandaa orodha ya wagonjwa wanaokosa kuhudhuria kliniki na kushirikiana na wahudumu pamoja na asasi zinazohusika ili kuwatafuta na kuwahimiza kurejea kupata huduma.
Kwa upande wake, Mtaalamu wa Afya ya Akili na Utengamao katika huduma ya MAT, Dkt.Ally Mapinda amesema,huduma ya Methadone imekuwa na mchango mkubwa katika kuwasaidia watu wenye uraibu, hasa wa heroini, kupunguza utegemezi wa dawa hizo na kujenga upya maisha yao kwa msaada wa wataalamu wa afya.
Amesema wanajivunia kwani baadhi ya waliopata huduma hiyo wameweza kurejea katika shughuli za uzalishaji, kusaidia familia zao na kuendelea na majukumu yao ya kijamii, wengine wameoa, wengine wamerudi kazini, wengine ni wavuvi, madereva na waendesha bodaboda.
Akizungumzia vifo vya baadhi ya wagonjwa waliosajiliwa katika huduma hiyo, Dkt.Mapinda amesema,vinaweza kusababishwa na sababu mbalimbali za kiafya na mazingira ya maisha ya wagonjwa, hivyo haviwezi kuhusishwa moja kwa moja na matumizi ya Methadone pekee.
Ameitaja changamoto ya kutumia dawa kupita kiasi na kuchanganya Methadone na vilevi vingine kuwa miongoni mwa hatari zinazoweza kuhatarisha afya na maisha ya wagonjwa, akiwataka wanaopata huduma hiyo kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.
Aidha, amesema magonjwa kama shinikizo la damu, kifua kikuu na ‘septicemia’ pamoja na ajali za barabarani ni miongoni mwa sababu za vifo vya baadhi ya wagonjwa.
Naye Mratibu wa asasi isiyo ya kiserikali ya Gift of Hope jijini Tanga, Said Bandawe amesema, wameona umuhimu wa kuandaa wakufunzi watakaotoa elimu katika maeneo mbalimbali ya kazi ili kuongeza uelewa kuhusu madhara ya dawa za kulevya, namna ya kujikinga na hatua za kuwasaidia walioathirika.
Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya dawa za kulevya hayawezi kufanikiwa kwa kutegemea Serikali au vyombo vya usalama pekee, bali yanahitaji ushiriki wa wazazi, vijana, waandishi wa habari na jamii kwa ujumla.


More Stories
TANESCO kuiwezesha HWTZ kuzalisha Megawati 200 za umeme
Mlowo yaanza kupangwa kisasa, 165 walipwa fidia
Wajumbe Mamlaka waridhishwa ujenzi wa shule mpya Mlowo.