Mwandishi wetu,Timesmajira,Online, Babati
Wanafunzi 40 wa shule za sekondari wilaya ya Babati,mkoa Manyara wametakiwa kuwa mabalozi wazuri wa Utalii na Uhifadhi,baada ya kupata fursa kwenda kutembelea kujifunza uhifadhi katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro(NCAA).
Wanafunzi hao wakiwa pamoja na walimu wao,Wazazi na baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji vinavyounda Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya Burunge,wameanza leo ziara ya mafunzo ya siku tano katika hifadhi hizo,ziara inayofadhiliwa na Taasisi ya uhifadhi ya Chem Chem Association.
Akizungumza wakati wa kuwaaga wanafunzi hao,Mkuu wa wilaya ya Babati,Hashim Shaibu Mgandilwa amesema wanafunzi hao baada ya kurudi wanapaswa kuwa mabalozi wazuri wa uhifadhi na Utalii.

Mgandilwa amesema, Tanzania imebarikiwa kuwa na hifadhi nyingi za Wanyamapori na mazingira hivyo ni wajibu wa kila mtanzania kuzitunza kwa manufaaya sasa na vizazi vijavyo.
“Sisi watu wazima tumeona faida ya uhifadhi sasa tunataka nyie wanafunzi mkirudi mkatowe elimu vijijini kuhusu kuendelea kutunzwa hifadhi zetu ili vizazi vijavyo vizikute na sio waje kukuta historia tu”amesema
Mkuu huyo wa wilaya alipongeza Taasisi ya Chem Chem ambayo pia imewekeza shughuli za utalii katika eneo la Burunge WMA kwa jitihada kubwa inayofanya kuendeleza uhifadhi na Utalii.
“Tumezoea kuziona taasisi nyingi zinaeleza kujikita kufanya mambo ya utetezi katika jamii lakini nyie mnafanyakazi ambazo zinaonekana na kupimika hivyo serikali inawaunga mkono”amesema.
Meneja Mkuu wa Chem Chem Association,Clever Zulu amesema programu ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi iliyoanza mwaka uliopita inalenga kuwajenga wanafunzi kujua faida za uhifadhi na Utalii na hivyo kushiriki katika kutunza mazingira na wanyamapori.
“Leo ujumbe wa wanafunzi watu 60 wakiwepo wanafunzi 40 utaanza ziara hii na tunaimani wanafunzi hawa wakirejea watakuwa mabalozi wa kutunza mazingira na uhifadhi kwani wakiwa ziara watakutana na wahifadhi na kupewa elimu ya uhifadhi na Utalii”amesema.
Mwenyekiti wa Burunge WMA,Paschal Shing’ida amesema ziara hiyo ni muhimu katika eneo lao kwani tayari kuna manufaa makubwa jamii inapata kutokana na uhifadhi na Utalii.
Baadhi ya wanafunzi wakizungumza na wanahabari walipongeza kuteuliwa kushiriki ziara hiyo na kuahidi wakirudi watatoa vizuri elimu ya uhifadhi,Utalii na kupinga ujangili vijijini na kuanzia katika familia zao.

More Stories
PPAA yaelimisha wabunifu, wakadiriaji kuhusu zabuni za umma
WHO yaipongeza Tanzania Bima ya Afya kwa Wote
Mchengerwa: Hakuna Mtanzania atakayekosa matibabu