October 21, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Madiwani viti maalumu jiji la Mbeya wakabidhi msaada wa chakula shule ya msingi Kambarage

Na Mwandishi wetu, Timesmajira, Online Mbeya

KATIKA kuhakikisha shule za msingi zinakuwa na chakula cha kutosha, Madiwani wa Vitimaalum Jijini Mbeya wameguswa kwa shule mbalimbali zilizopo jijini hapa na kukabidhi msaada wa chakula kwa shule ya Kambarage na Ikuti, lengo likiwa ni kuwaunga mkono wazazi ambao wamekuwa wakichangia chakula kwa ajili ya watoto.

Akizungumza Oktoba 20, 2026 kabla ya kukabidhi chakula katika shule ya Msingi Kambarage, mmoja wa Madiwani wa Vitimaalum Jiji la Mbeya, Fatuma Bora, amesema kuwa kama wazazi wamekuja na chakula ili kuweza kuwapa hamasa watoto waweze kuwa na bidii ya kusoma na kujituma

.

“Chakula hichi kiwape upendo na hamasa kwa sababu kuna wazazi ambao hawajatoa mchango. Wewe mzazi ambaye umetoa mchango wa chakula, hebu mshike mkono mwenzako, mwambie kula na usimpe chakula mwenzio kama adhabu. Mungu hapendi. Naomba watoto msikubali kupewa zawadi kwa mtu yeyote ambaye hamjujui,” amesema Bora.

Aidha Bora amesema kuwa lengo la Madiwani wa Vitimaalum ni kuwasapoti wazazi kwa sababu wazazi ndio wanaleta chakula, hivyo Madiwani wameweza kupata udhamini kutoka kwa wadau ili kuweza kuona umuhimu wa kuchangia chakula.

Mariam Kikasi, Diwani Vitimaalum Jiji la Mbeya, amewataka watoto kutokubali kufanyiwa vitendo vya ukatili na kutosita kutoa taarifa pale inapobidi kufanyiwa vitendo hivyo.

“Tunawasihi watoto wetu msihadaike kwani vipo vitendo vingi vya ukatili na hamsemi. Mkipata wasaa mzungumze ili msipoteze malengo yenu ya baadaye. Kama mzazi yupo bize, ongea na mwalimu au jirani, msikae na vitu moyoni. Vipo vitendo vingi pia, watoto wa kiume msikubali kufanyiwa hivyo vitendo,” amesema Diwani huyo.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Kata ya Ruanda, Jane Mwakwenda, amesema kuwa kitendo cha Madiwani hao kujitoa kuchangia chakula kitaleta hamasa kwa baadhi ya wazazi wasiokuwa na mwamko wa kuchangia chakula kuweza kuchangia.

“Wanangu wazuri, si mmeona hawa wageni wetu walivyojitoa kutuleta chakula hapa shuleni Kambarage? Hivyo na nyinyi mkifika nyumbani mkawambushe wazazi kuchangia chakula kwani ni uhai ambao unamfanya mtoto kusoma kwa bidii pale anapokuwa ameshiba,” amesema Afisa Elimu huyo.