October 20, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Burhan ataka UVCCM kurejea misingi kuanzishwa kwake


Na Joyce Kasiki, Dodoma



KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Faris Buruhani, amesema vijana wa jumuiya hiyo wanapaswa kurejea na kusimamia misingi ya kuanzishwa kwake ili kuimarisha chama, kuzalisha viongozi bora na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa.


Buruhani amesema hayo jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na vijana waliojitokeza kumpokea katika Ofisi za Makao Makuu ya UVCCM, kufuatia uteuzi wake wa kushika nafasi hiyo.


Amesema kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa UVCCM, Mohammed Ali Kawaida, pamoja na viongozi wengine wa jumuiya hiyo katika ngazi zote, atahakikisha taasisi hiyo inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi iliyowekwa tangu kuanzishwa kwake.


Buruhani amesema Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatamani kuona UVCCM ikiendelea kuishi kwa kuzingatia misingi yake, akiahidi kuwa viongozi wa jumuiya hiyo watasimamia maono hayo kwa vitendo.


“Tutahakikisha tunajitahidi kwa kiasi kikubwa kuona jumuiya yetu inarudi na kuishi katika misingi ya kuanzishwa kwake,” amesema Buruhani.


Ametaja misingi hiyo kuwa ni kuwaunganisha vijana wa Kitanzania, kuwajengea uelewa wa itikadi na sera za chama, kuwashirikisha katika shughuli za CCM na kuwaandaa kushiriki katika uongozi ndani ya chama na Taifa.


Kuhusu suala la itikadi, amesema UVCCM itaimarisha programu za mafunzo kwa vijana kupitia vyuo na maeneo maalumu ya kufundishia itikadi ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa sahihi wa chama chao.


“Tutahakikisha vijana wa CCM hawawi vijana wa kuangalia shughuli za chama tu, bali wanakuwa vijana wanaokijua chama chao na kuelewa itikadi yake,” amesema.


Aidha, amesisitiza umuhimu wa vijana kulinda maslahi ya taifa, akisema Tanzania ni urithi walioachiwa na wazee wao katika hali ya amani, usalama na utulivu, hivyo kila kizazi kina wajibu wa kuilinda.


Amesema masuala ya kitaifa yanapojadiliwa, vijana wanapaswa kuweka mbele maslahi ya nchi badala ya tofauti za kisiasa ili kudumisha amani na mshikamano.


Katika hatua nyingine, Buruhani ameiomba CCM kuchunguza tuhuma za rushwa zinazodaiwa kuwakabili baadhi ya vijana ili ukweli ubainike na haki itendeke.


Amesema uchunguzi huo unapaswa kufanyika kwa kufuata katiba, kanuni na taratibu za chama, akieleza kuwa hatua stahiki zinapaswa kuchukuliwa endapo tuhuma hizo zitathibitika.
“Kama kweli tuhuma hizo zina ukweli, basi hatua zichukuliwe kwa mujibu wa utaratibu. Vilevile, kama tuhuma hizo hazina ukweli, hatua zichukuliwe kwa mujibu wa taratibu za chama,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Bara, Mussa Mwakitinya, amesema ujio wa Buruhani katika nafasi hiyo unaungwa mkono na vijana, akiahidi kuwa wataendelea kushirikiana naye katika kuimarisha shughuli za jumuiya.


Mwakitinya amesema uteuzi huo umeweka matarajio makubwa kwa vijana, akimtaka Katibu Mkuu huyo kutumia nafasi yake kuendeleza ujenzi wa CCM na kuimarisha ushiriki wa vijana katika shughuli za chama.