October 19, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yaendelea kudhamini ‘Yas Kili Half Marathon’

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya Yas Tanzania,  imethibitisha kuendelea kudhamini mbio za kilomita 21 za “Yas Kili Half Marathon” huo ukiwa ni mwaka wa 13 mfululizo. Mbio hizo ni sehemu ya Kili International Marathon zinazotarajiwa kufanyika mwakani Februari 07, 2027 mkoani Kilimanjaro.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa msimu wa 25 wa Kili International Marathon mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Mstaafu  Kassim Majaliwa amesema mashindano hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa kukuza vipaji vya wanariadha na kuitangaza Tanzania kupitia utalii wa michezo.

“Miaka 25 ni mafanikio makubwa kwa mbio hizo na yanaonyesha uthabiti, maono na ushirikiano mzuri kati ya waandaji, wadau na Serikali ya Tanzania”, amesema Majaliwa.

Ameongeza kuwa, mbio hizo zimewapa wanariadha wa Tanzania nafasi ya kujipima na kupata uzoefu wa kushindana na wakimbiaji kutoka mataifa mbalimbali.

Amewataka wadau kuendelea kuwasaidia wanariadha wa ndani ili kuongeza ushindani wao katika mashindano makubwa.

Majaliwa pia amesema, ujio wa mbio hizo unachochea uchumi wa Tanzania na kutoa fursa kwa wafanyabiashara mbalimbali mkoani Kilimanjaro na maeneo ya jirani kuingiza kipato.

Amewahimiza washiriki kuwa licha ya kukimbia basi watumie fursa  hiyo kutembelea vivutio vya utalii vinavyopatikana mkoani Kilimanjaro.

Kwa upande wake, Meneja wa Chapa na Mawasiliano- Yas Tanzania, Woinde Shisael amesema wanajivunia kuendelea kuwa sehemu ya mbio hizo kwa mwaka wa 13 mfululizo kutokana na mchango wake katika kuhamasisha afya, kukuza utalii wa michezo na vipaji vya wanariadha. Lakini pia,  kuleta fursa za kiuchumi kwa wakazi wa Moshi na Tanzania kwa ujumla.

Kaulimbiu ya Yas mwaka huu “Mbio za Viwango hadi kileleni” inawahakikishia washiriki wote kupata uzoefu (experience) yenye viwango vya kimataifa huku wakifurahia mtandao swadakta wa viwango.

“Kauli  mbiu hii inaenda sambamba na utambulisho mpya wa mtandao wetu ‘Mtandao wa Viwango’ baada ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Kampuni ili kuboresha huduma za mawasiliano.

“Washiriki wanahitaji mtandao wenye kasi na unaopatikana kwa uhakika ili kuendelea kuwasiliana na familia na marafiki, pamoja na kufuatilia shughuli zao mbalimbali wakiwa Moshi,” amesema.

Shisael amesema, kampuni hiyo pia itaendeleza utamaduni wake wa upandaji miti kando kando ya mlima Kilimanjaro na kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira ili kusaidia kulinda ikolojia na uoto wa Mlima Kilimanjaro.

“Mwaka jana tulifanikiwa kupanda miti zaidi ya 65,000 na kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wanajamii, wakiwemo wanafunzi. Tutaendelea na utamaduni huu katika mbio za mwaka 2027,” amesema.

Amewapongeza waandaaji, Wild Frontiers Events, pamoja na wadhamini wenza kwa kuendeleza mashindano hayo kwa miaka 25, huku akiwahimiza wakimbiaji wa ndani na nje ya nchi kujisajili mapema kupitia Mixx na kuanza maandalizi.