Na Penina Malundo,TimesMajira
MTANDAO wa Kupinga Ukatili dhidi ya Wanawake nchini Tanzania umelaani mauaji ya wanawake na wasichana, ukitaka Serikali kuimarisha mifumo ya ulinzi na utekelezaji wa sheria ili kuzuia vitendo hivyo.
Mtandao huo umesema wivu, migogoro ya kimapenzi au uamuzi wa mwanamke kusitisha uhusiano haviwezi kuwa sababu za kuhalalisha mauaji, ukisisitiza kuwa kila mwanamke ana haki ya kuishi kwa usalama.
Akisoma tamko la mtandao huo leo jijini Dar es Salaam, Neema Abeid amesema mauaji ya wanawake, yanayojulikana kama femicide, ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu unaohitaji hatua za haraka na za pamoja.
Amesema takwimu za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) zilizotajwa katika tamko hilo zinaonesha kuwa utafiti uliofanyika katika mikoa mitano ulirekodi matukio 50 ya mauaji mwaka 2023, ambapo wanawake walikuwa waathiriwa 45.
Abeid amesema takwimu hizo zinaonesha umuhimu wa kutambua viashiria vya ukatili mapema na kuchukua hatua za kinga kabla vitendo hivyo havijasababisha vifo.
Kwa upande wake, Nasra Mohamed ameitaka Jeshi la Polisi na vyombo vya uchunguzi kuchukulia kwa uzito taarifa za vitisho vya kuua, vipigo na unyanyasaji ili hatua za ulinzi zichukuliwe kwa wakati.
Amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama zinapaswa kuhakikisha kesi za mauaji na ukatili dhidi ya wanawake zinashughulikiwa kwa weledi, bila upendeleo na kwa kuzingatia sheria, huku haki za waathiriwa na familia zao zikilindwa.

Naye Alua Mkilindi ametoa wito kwa asasi za kiraia, viongozi wa dini na mila pamoja na vyombo vya habari kuimarisha elimu kuhusu ukatili na kutoa msaada wa kisheria, ushauri nasaha na hifadhi salama kwa wanawake walio katika mazingira hatarishi.
Amesisitiza kuwa wanaume na wavulana wanapaswa kushiriki katika kupinga fikra za umiliki na udhibiti wa wanawake, huku wananchi wakihimizwa kuripoti mapema vitisho na vitendo vya ukatili ili kuwezesha hatua za kinga kuchukuliwa.

Mtandao huo pia umetaka kuwepo kwa mfumo madhubuti wa kitaifa wa kukusanya na kuchambua takwimu za mauaji ya wanawake ili kubaini sababu za matukio hayo, vihatarishi na hatua zilizochukuliwa kabla ya mauaji kutokea.
Umeeleza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, vyombo vya sheria, taasisi za kiraia na jamii ni muhimu katika kuzuia mauaji, kulinda maisha ya wanawake na kuhakikisha wanaishi bila hofu ya kufanyiwa ukatili.

More Stories
UBA TANZANIA yazindua mfumo mpya wa malipo ‘PAPSS’
Ndejembi:Mradi wa TAZA kuchochea Maendeleo
Afrika yatathmini mikakati ya kuimarisha usafiri wa majini